MINARA 755 kati ya 758 ya mawasiliano ya simu imekamilika na tayari inafanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kukamilika kwa minara hiyo kumeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti, hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini na pembezoni.
Kupitia minara hiyo, wananchi sasa wanapata mawasiliano ya uhakika yanayowawezesha kuwasiliana kwa urahisi, kufanya miamala ya kifedha kwa njia ya simu, kupata taarifa muhimu, pamoja na kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi kama elimu, afya na biashara.
Utekelezaji huu unaendelea kuimarisha ujumuishaji wa kidijitali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo husika.
Kukamilika kwa minara hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wengi zaidi, huku minara iliyosalia ikiendelea kukamilishwa ili kufikia lengo la mradi kwa asilimia mia moja.