IMEELEZWA kuwa, Kampuni ya Uchimbaji dhahabu ya Geita Gold Mining Limited ( GGML) inaongoza kwa kuwa kampuni ya uchimbaji madini nchini inayofanya vizuri katika kutimiza Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (CSR).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alipotembelea mgodi wa GGM ili kushuhudia miradi mipya ya uchimbaji dhahabu inayofanyika katika mgodi huo Mkoani Geita.
“Mimi ningependa tuwe wa kweli, nchi hii kampuni inayofanya vizuri kwenye CSR kwenye madini ya kwanza ni GGM. Wamefanya kazi nzuri,” alisisitiza Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na wananchi katika huduma mbalimbali kwa jamii zinazozunguka migodi hususan, katika ujenzi wa hospitali, shule, vifaa vya tiba ili jamii ipate huduma bora.
Aidha, ameipongeza GGM kwa kujenga mahusiano mazuri ya kijamii na wananchi wanaozunguka mgodi huo. Dkt. Biteko amepongeza GGM kwa kuweka mitambo mipya ya kuchenjua mabaki ya kaboni ili kupata dhahabu badala ya kusafirisha kaboni kwenda nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo kabla.
Vile vile, mgodi wa GGM umeanza kuhama katika uchimbaji wa wazi na kwenda kwenye uchimbaji wa chini kwa chini (underground mining), ambapo tayari GGM imejenga mgodi wa chini ya ardhi na umeanza uzalishaji.
“Tunafurahi kuona kwamba mgodi wa GGM wamejitaidi kuendelea kuweka uzalishaji kuwa kwenye kiwango kinachotakiwa. Kwa mujibu wa taarifa za mgodi, mgodi huo unazalisha Wakia 480,000 hadi sasa, tunawapongeza sana,” alisema.
Alisema, Serikali inaandaa Kanuni na Muongozo maalum ambao utawafanya watu wote watekeleze miradi ya kijamii bila kutegea nchini.
Naye, Makamu wa Rais wa Kampuni ya GGM, Simon Shayo akizungumzia kuhusu utekelezaji wa CSR kwa jamii amesema, kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri katika mazingira yote yanayozunguka mgodi.
Pia, alimshukuru Dkt. Biteko kwa kuipongeza GGM kwa namna kampuni hiyo inavyojitaidi kwenye kununua bidhaa na kutumia huduma za kitanzania.
“Asilimia kubwa ya bidhaa zetu sasa karibu asilimia 70 ya fedha inayotumiwa na GGM inanunua bidhaa kutoka Tanzania,” alisisitiza.
Shayo alisema, lengo la kampuni ya GGM ni kuhakikisha kuwa inaendelea kuwa kinara kwa kufanya vizuri ili watu wavutiwe kuwa mwajiriwa wa GGM na wote wanaozunguka mgodi huo kuwa na ujirani wa manufaa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Geita, Costantine Kanyasu alisema, lengo ni kuona wananchi wanashiriki katika uchumi wa mgodi.
Alisema, katika maeneo mengi ya jimbo hilo mgodi unashirikiana na wananchi wake na kusisitiza kuwa jimbo linapokea asilimia 54 ya fedha ya CSR inayotengwa na kuzielekeza katika huduma za maendeleo.