Mchengerwa: Rais Samia ni zao la jitihada za Bibi Titi

0
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa.

Na Jumbe Abdallah

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema taifa linajivunia utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia Suluhu ambaye ni zao la hamasa ya Hayati Bibi Titi Mohamed katika kuwahamasisha wanawake nchini kushika nafasi za juu za uongozi.

Mchengerwa amesema hayo jijini Dar es Salaam baada ya dua ya kumuombea Hayati Bibi Titi iliyofuatiwa na uzinduzi rasmi wa Tamasha la Kumbukizi la Bibi Titi kwa mwaka 2023 (Bibi Titi Memorial Festival 2023).

Mchengerwa alisema, Bibi Titi alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na alifanya kazi kubwa ya kumsaidia Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kulikomboa taifa.

“Marehemu Bibi Titi Mohamed alikuwa jasiri na kupitia nafasi yake katika chama alifanikiwa kupenyeza habari za ukombozi wa taifa kwa watanzania wengi na kujenga ujasiri miongoni mwa wanawake akiwahimiza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,” alisisitiza Mchengerwa.

Aliongeza kuwa “Ndoto za Bibi Titi zilikuwa ni kuona siku moja wanawake wakishika nyadhifa za uongozi wa ngazi za juu kama ilivyo sasa, ambapo tuna Rais mwanamke, Spika wa Bunge mwanamke, Mawaziri wanawake, Makatibu wakuu na Wakurugenzi wanawake katika taasisi mbalimbali.”

Kuhusu tamasha la Bibi Titi kwa mwaka 2023, Waziri Mchengerwa amesema tamasha hilo linalojumuisha zaidi ya vikundi 200 vya mbio za polepole (Jogging club) kwa mwaka huu (2023) litatumika zaidi kukieleza kizazi cha sasa kuhusu mchango wa Bibi Titi Mohamed kwenye ukombozi wa taifa kwa kuwa vijana waliowengi bado hawajui historia yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here