Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Zanzibar hakuna njaa, wala upungufu wa bidhaa muhimu za vyakula au bei za bidhaa kuwa juu kwenye Masoko kama inavyodaiwa na upinzani.
Kadhalika chama hicho kimetaja shida kubwa iliyopo Zanzibar ni upinzani kutaka kutamani madaraka kwa kutumia mbinu batili, uzushi na uongo.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis, alipomaliza kutembelea Soko jipya la Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi Kisiwani Unguja.
Mbeto alisema, maisha ya wananchi kwa ujumla yanaendelea kama kawaida, bei za bidhaa ni wastani, wafanyabishara wanafanya shughuli zao, hakuna aliyepandisha bei kama inavyopotoshwa kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema, njaa ya Zanzibar ni ya kisiasa huku wapinzani wa CCM wakitamani madaraka kwa kutumia hila, uongo na uzushi kwa kudai Zanzibar kuna maisha magumu.
“Zanzibar kuna njaa ya kisiasa, upinzani unalilia madaraka kwa kutumia sera zisizoungwa mkono na wananchi. ACT wanalilia kushika utawala bila kuwavutia wananchi kwa sera makini. Badala yake wanategemea nguvu za uzushi, unafiki na uongo ” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi, alisisitiza kuwataka viongozi wa ACT kuelewa utendajikazi uliofanywa na Serikali ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa miaka minne, umejenga imani kwa wananchi baada ya kutimiza ahadi zilizoahidiwa kupitia ilani ya uchaguzi na kuleta maendeleo.
“Kila kilichoahidiwa kwenye ilani na ahadi za Rais Dkt. Mwinyi mwaka 2020 zimetimizwa hatua kwa hatua na kwa wakati sahihi. SMZ haikutaka kuendekeza malumbano ya kisiasa majukwaani badala yake iliweka mkazo kusimamia mabadiliko ya kimaendeleo,” alieleza.
Mbeto alisema, takribani Masoko yote yamesheheni bidhaa muhimu kwa ajili ya maisha ya kawaida pia kuna aina zote za vyakula kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Hata hivyo, Mbeto aliwaasa ACT na kuwataka waache siasa za kizushi, zinazokuza mifarakano katika kijamii ilihali wakijua zama hii si zama ya kutegemea udaku, uzushi na uongo kama mtaji wa kisiasa kwa chama makini cha siasa.