Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema ACT Wazalendo kitapata pigo kubwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi atashinda kwa kishindo kutokana na maandalizi yanayoendelea kufanyika.
CCM kimewahakikishia wananchi wa Pemba kuwa, mgombea urais wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman hana ubavu wa kumshinda kiongozi aliyeiletea Mageuzi ya kimaendeleo Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis, aliyesema nguvu ya umma ndio itakayomrudisha tena Rais Dkt. Mwinyi madarakani.
Mbeto alisema, uchaguzi wowote ili chama cha siasa kiweze kushinda ni mpango wa maandalizi na mikakati kabambe si mbwembwe, fedhuli wala mikogo.
Alisema, CCM kinaamini kazi kubwa ya mikakati ya kimageuzi kuelekea maendeleo ya kweli Zanzibar, imefanywa na Rais Dkt. Mwinyi kwa jinsi anavyoendelea kuitumikia Zanzibar.
“ACT kiseme na kuonyesha kimefanya nini katika kuwatumikia wananchi .Kiache kulitaja jina la Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kama mtaji wa kupata kura. CCM kimetenda na yaliofanyika yanaonekana kwa macho,” alisema Mbeto.
Akijibu madai yaliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Ismail Jussa Ladhu akiwa jimbo la Mtambwe, aliyedai ACT kitashinda Uchaguzi, ajiandae kushuhudia kikipeperushwa na kimbunga Hidaya.
“Jussa ndiye mgombanishi mkubwa baina ya viongozi wenzake na Hayati Maalim Seif. Wewe Jussa ni kirusi hatari na mchafuzi wa mahusiano toka mkiwa CUF na sasa amkiwa ACT”, alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alimtaka Jussa asimame kama Mwanasiasa mwenye uwezo wa kujieleza na kushawishi wananchi kwa sera za chama chake na kuacha kukitumia jina la Maalim Seif kwani sio sera wala maendeleo.
“CCM haina kabrasha la makubaliano yoyote yaliyofanyika kati ya Rais Dkt. Mwinyi na Maalim Seif. Kama Jussa ana ushahidi huo auonyeshe na kutaja yalioazimiwa, lini na wapi yalikofanyika,”alieleza.
Hivyo basi, Mbeto alimtaka Makamu huyo Mwenyekiti ACT aache maneno ya kutunga na kutamka maneno ya kipuuzi na yenye ujinga mwingi.
“Jussa huna siri zozote unazozijua za Maalim Seif katika siasa za Zanzibar bali wewe ni mzandiki na mzushi baada ya Maalim Seif kufariki na kuzikwa kwa heshima zote,” alisema.
Mbeto aliwataja baadhi ya wanasiasa ndani ya ACT ambao walikuwa karibu na Maalim Seif ni kina Hamad Rashid Mohamed na Juma Duni Haji lakini si yeye mtoto wa watu,” alisisitiza Mbeto.