Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimetaka utii katika viapo na viongozi na wanachama kujizuia na matamko majukwaani ili kutoiyumbisha kiutendaji kamati ya pamoja baina ya chama hicho na ACT Wazalendo.
Kamati hiyo imepewa jukumu la kujadili na kutoa mapendekezo agenda za utekelezaji wa tamko la pamoja la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari waliotaka kujua msimamo wa ofisi yake hadi kufikia hatua hiyo, Katibu wa Kamati Maalum (NEC), Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema, ni vema viongozi kujitahidi kujizuia na matamko ili kutoharibu mchakato mzima wa jambo hilo.
“Viongozi tujizuie kutoa matamko mbalimbali ili tusiharibu mchakato mzima wa hili jambo, sio rahisi atokee mwenzetu aseme mambo sivyo tutamjibu na tukianza hatua hiyo kujibizana sasa tutaharibu au tuyawayumbisha wajumbe wetu,” alisema Mwenezi Mbeto.
Alibainisha kuwa, kamati hiyo ya pamoja imekabidhiwa kazi kubwa ya kuifanya na baadae walete matokeo na mapendekezo kwa ajili ya kutekelezwa na chombo kingine ambacho kitaundwa kisheria.
Hivyo kamati hiyo inatimiza takwa la tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya CCM na ACT Wazalendo lililosainiwa Julai 9, 2026, Ikulu Zanzibar na kuwataka waweka mbele maslahi ya nchi na sio utashi binafsi.
Mbeto alisema, CCM inaunga mkono jitihada zote na kitatoa ushirikiano kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Dkt. Othman Masoud Othman ambaye ameapa kwa Katiba ya Zanzibar kuwa atashauri Rais kwa uaminifu na uadilifu na hatatoa siri za Baraza la Mapinduzi au za Serikali.
“Kwa hiyo tunaomba tuishi katika viapo vyetu na tuvisimamie viapo ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa salama yenye umoja, mashirikiano na kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi zaidi” alisema.
Komredi huyo alisema hadi kufikia hatua hiyo haikuwa jambo rahisi na kwa busara za CCM na za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi imewezekana.
Mbeto alibainisha kuwa, SUK Kitaifa ni takwa la Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kulingana na Mabadiliko/Maboresho ya 10 ya 2010 ya Katiba ambapo Ibara ya 9 Kifungu kidogo 1 kinataja uwepo wa SUK.
”Ibara ya 39 kifungu cha 1,2 kinaelezea upatikanaji wake Makamu wa Kwanza, wa pili wa Rais na kifungu kidogo cha 9 katika Ibara hiyo kinaelezea kuwa lazima awe na sifa ya Mwakilishi,” alisema Mwenezi Mbeto.
“Kwa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Rais atashauriana na chama husika kilichoshika nafasi ya pili kutoa jina au kuteua jina la Makamu wa Kwanza na Ibara ya 39 kifungu cha 1,2, 3 hadi 9 pamoja na mambo mengine vinaelezea pia mgawanyo wa nafasi za mawaziri” alisema Mbeto.
Alisema kuwa baada ya uchaguzi mkuu uliopita 2025. ACT Wazalendo ambao waliukuta mfumo huo wa kikatiba ulioanza CUF, waligomea kujiunga SUK wakidai baadhi ya taratibu zilikiukwa katika uchaguzi mkuu uliopita na mambo mengine ndani ya umoja huo wanayotaka yaangaliwe upya.
Mwenezi Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi, akawaomba marais wastaafu, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Mohamed Ali Shein kuwasikiliza na kati ya mambo hayo ndio hizo agenda ambazo kamati ya pamoja inaenda kuzijadili na kutoa mapendekezo.
Kulingana na hadidu rejea, mapendekezo hayo atakabidhiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Mwinyi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo, vyama vyote viwili vya siasa kwa ajili ya kuzipitia kisha muswada utapelekewa Baraza la Wawakilishi ili kutunga Sheria ya kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia utekelezaji.