Mbeto: Si Lissu wala Heche kwa Dkt. Samia 2025

0

KATIBU Kamati Maalum NEC, Zanzibar, Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema, ni vigumu kwa wananchi kusikiliza propaganda za viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa hakuna maendeleo yaliyopatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari Visiwani Zanzibar leo, Machi 25, 2025, Mbeto alisema chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mafanikio yamepatikana kwa kila sekta.

“Wakati tunapata uhuru 1961 asilimia 70 ya watanzania walikuwa hawajui kusoma wala kuandika, leo asilimia 83 wanajua yote mawili,” alisema.

Alibainisha kuwa, hivisasa kila kata ina shule ya sekondari, pia sera ya elimu na mafunzo ya 2014, toleo la 2023 inabainisha kuwapa uwezo vijana katika elimu na stadi kikabili ushindani kikanda na kiulimwengu.

“Tuna vyuo vikuu 35 na 15 vishiriki, utasemaje hakuna maendeleo?,” alihoji na kuongeza kuwa, ulimwengu unatambua jitihada za Dkt. Samia katika masuala ya kijamii na usalama.

Alisema, Tuzo ya Kimataifa ya Goalkeeper Award ya Gates Foundation na mkutano wa SADC na EAC kuhusu DR Kongo vimempa heshima yeye binafsi na Taifa kwa ujumla.

“Kafanya mengi sana ambayo ni historia katika nchi na ulimwengu kwa ujumla ikiwemo mikataba yenye tija kwa Taifa. Maendeleo ni hatua na wananchi wanayoyaona wanayafurahia,” alisema Mbeto.

Aliendelea kusema, pamoja na mambo mengine, Rais Samia ameonyesha uungwana kwa kuridhia takwa la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) la kuwepo kliniki za kisheria ambazo hadi sasa zinazunguka nchi nzima.

Mbeto amebainisha kuwa, upinzani utasubiri sana kwani mengi yanafanyika na kubwa zaidi kuufungua mkoa wa viwanda Tanga kwa kuweka mikakati kufufuliwa viwanda vilivyokuwepo, upanuzi na ujenzi wa Bandari ya Tanga na umeme wa uhakika wenye msongo mkubwa kutoka Ethiopia.

“Lissu na Heche hawajielewi hata Chadema yenyewe ipo vipande vipande na hawana hoja za kuwaeleza watanzania, kwa maana hiyo hawawezi kushindana na Dkt. Samia kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here