Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
IDARA ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, imemtaja Mwenyekiti wa ACT, Othman Masoud Othman hakuwahi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura na wala kuwa mpiga kura mwaka wowote.
Mara kadhaa, CCM kimemtaja Othman si kwamba hajawahi kujiandikisha tu, lakini pia hakuna rekodi inayoonyesha kama amewahi kupiga kura katika jimbo lolote.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alisema jina la Othman halionekani katika orodha ya wapiga kura walioandikishwa kuanzia mwaka 1995 hadi 2025.
Mbeto alisema kilichofanyika huko Mpendae, amekwenda kujiandikisha na kama mpiga kura mpya, wakati zoezi la wapiga kura kuhakiki na kurekebisha taarifa zao limeshafanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Julai Mwaka 2020.
Alisema, kutoonekana jina la Othman katika orodha ya wapiga kura wa zamani, kunaweza kuthibitisha kuwa kiongozi huyo hajawahi kumpigia kura mgombea urais kwa tiketi ya ACT Hayati Maalim Seif
“Si jambo la kupepesa maneno ila ni rahisi kusema Othman ni aina ya kiongozi asiye na msimamo. Si kosa kisiasa akiitwa mwenye rangi za mwanasiasa kinyonga au mchumia tumbo,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, madai yaliyotolewa na Jussa na kudai Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye aliyempendekeza Othman kurithi uongozi wa ACT ni mbinu batili na uongo mtupu.
“Hawezi kupendekezwa mtu ambaye hakushiriki harakati zozote za kuijenga CUF au ACT. Othman amedandia siasa za ACT kwa mbinu na mizengwe iliyosukwa na Jussa akiwa na wenzake wake saba,” alieleza.
Aidha, Mbeto aliongeza kusema hata katika jimbo la Mpendae, Othman amenunua nyumba tu, lakini kwa miaka yote hakuwahi kuwa Mkaazi wa kudumu wa eneo hilo kama sheria ya Ukaazi Namba 4 ya mwaka 2018 inavyoelekeza.
“OMO amekosa hata sifa ya kuwa mpiga kura mpya . Huu si wakati wa kurekebisha tarifa walioandikishwa kupiga kura .Kwa muktadha huo hakuwahi kumchagua hata aliyekuwa bosi wake Rais Mstaafu Dk Ali Mohamed Shein wala Maalim Seif “Alieleza .
Akizungumzia madai yaliowahi kutolewa na Jussa huku akisaidiwa na mjane wa Maalim Seif, Bi Awena Sinani, ikidaiwa kuna usia ulioachwa na Hayati Maalim Seif, unaompendekeza Othman awe kiongozi ACT jambo hilo ni uzushi mtupu.
“Ni lazima vyama vyetu viwe makini kudhibiti viongozi matapeli wa kisiasa.Huenda ameihukumu sana SMZ na sasa anakitafuna,” alisisitiza Mbeto.
Alisema, hata Hati ya kusafiria ya OMO haionyeshi kama mwaka 2020 aliwahi kusafiri na kukaa nje ya Zanzibar zaidi ya miaka mitatu, hivyo bado anaonekana kutothibitika kuwa mpiga kura halali.