Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAMATI Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo imemuasa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kuepuka fikra zozote za kutamani kurithi sera za Kiongozi wa zamani wa UNITA, Jonas Savimbi.
Aidha, azma ya kufikia uamuzi wa kutaka kuweka kando maridhiaono ya kisiasa Zanzibar na kuanzisha mapambano, anaweza kuitia hofu dunia na kuanza kumtazama kwa jicho lenye shaka
Hayo yameelezwa na Katibu wa Idara hiyo ya CCM upande wa Zanzibar, Khamisi Mbeto Khamis, aliyesema fikra zozote za kutishia kuvunja maridhiano ya kisiasa, inakusudia kuchochea fujo na ghasia kuelekea oktoba mwaka huu.
Mbeto alisema, ni wazi Othman ameshindwa kukiongoza ACT kwa siasa za kisasa, badala yake kauli zake zinavunja misingi ya demokrasia kwa kutamani urithi wa sera za mapambano.
Alimtaka Mwenyekiti huyo wa ACT kujua siasa za mapambano zimepoteza maisha ya watu wengi huko Angola na Msumbiji wakati wakipigania uhuru.
“Hadi kiongozi wa kisiasa anapotangaza uamuzi wa kutamani mapambano anaelekea kuingia msituni . Kwa Zanzibar sijui atajificha msitu upi kati ya Jozani na Ngeezi. Ni wazi ACT kinazidi kupoteza haiba na amana yake kisiasa kwa kuiga mrengo hasi na batili,” alisema Mbeto.
Alisema, kabla ya kuchaguliwa Mwenyekiti wa ACT, Mbeto alisema Othman hakuwa Mwanasiasa, bali ni msomi nguli wa sheria ambaye sasa inathibitika anapungukiwa na uwezo wa kukiongoza chama chake.
Mwenezi huyo wa CCM alisema, katika maisha yake ya siasa Hayati Maalim Seif Sharif Ahmad ametembea dunia nzima, lakini hakukutana na mkasa wa kuzuiwa kwenye uwanja wowote wa ndege duniani.
“Viongozi wa ACT wanajua amepata nafasi ya uenyekiti kwa mizengwe ya Makamo wake Mwenyekiti, Ismail Jussa Ladhu si ridhaa ya wana ACT .OMO anaishi ACT lakini wenye chama hawamkubali,” alieleza.
Mbeto aliongeza kusema, hatua yoyote kwa Mwanasiasa yeyote anayetaka kuiingiza Tanzania kwenye machafuko au kurudisha tena matukio ya ulipuaji mabomu, watu kumwagiwa tindikali, viongozi wa dini kuuwawa au kutiwa vilema, dola ipo itatimiza wajibu wake.
“Kiongozi mwanademokrasia hawezi kutamka anaweka kando siasa za maridhiano na kujiandaa kwa mapambano. Matamko hayo ni sawa na kutangaza janga la uhalifu,” alisisitiza Mbeto
Hata hivyo, alisema vyama vyote vya siasa nchini, vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria Namba 5 ya Mwaka 1992, vitashindanisha sera na kubadilishana madaraka kupitia demokrasia ya uchaguzi si kimapambano.