Mbeto: Kauli ya Othman ni tangazo la fujo Zanzibar

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema matamshi yaliyotamkwa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, akidai muda wa maridhiano umepita, sasa ni wakati wa mapambano ni tangazo la fujo kabla ya Oktoba mwaka huu.

Aidha, CCM kimeyaita matamshi hayo yanachochea vurugu, ukorofi na ubabahifu kuelekea uchaguzi mkuu 2025, baada ya ACT kubaini hakina nafasi ya kushinda.

Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, ambapo alifafanua kuwa, maridhiano ya kisiasa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar yamefikiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Mbeto alisema, Zanzibar kwa takriban miaka mitano chini ya utawala wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wananchi wamekuwa wakiishi kwa amani, umoja na maelewano tofauti na kabla ya wakati wa maridhiano kufikiwa.

Alisema, maelewano yaliyopo Zanzibar ni baada ya kufikiwa na miafaka kadhaa, hatimaye ndipo maridhiano yaliyoridhiwa na vyama vya CCM na CUF mwaka 2009 yakaunda SUK.

“Bila shaka Othman hatambui maridhiano ya CUF kwakuwa ACT sicho kilichofikia muafaka. Hata hivyo msimamo huo ni aina ya chochezi mpya . Ikiwa ACT kuna fukuto na mvutano asihamishie matatizo hayo kwa wananchi,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, wananchi toka mwaka 2010 wamekuwa wakiishi kwa maelewano imara, hivyo hawako tayari kugawanywa kwa namna yoyote na kuirudisha nyuma Zanzibar kimaendeleo.

Mbeto alisema, hata matamshi ya Othman kumtaja mkuu wa nchi mwanamke na kumwita mwizi, hayampi heshima Mwenyekiti huyo wala chama chake mbele ya jamii inayomtazama.

“Kumtaja kiongozi mwenzako kwa jinsia yake ya kike au kiume ni kebehi na dharau. Othman kama atakuwa ndiye mgombea urais wa ACT ameshindwa kabla ya Oktoba mwaka huu,” alieleza

Mbeto alisema, hatua ya ACT Wazalendo kudai kitaongoza mapambano na kuweka kando maridhiano, hakionyeshi nia njema na ukomavu wa kisiasa badala yake chama hicho kimejipanga kwa fujo.

“ACT Kutangaza hakitaki siasa za maridhiano badala yale kitaendesha siasa za mapambano ni ukiukaji wa matakwa ya misingi ya demokrasia. Matamshi ya ACT yanavunja azma ya kulinda umoja na amani,” alisema.

Mbeto alisema, hata kukitaja kikao cha Kamati Kuu ya ACT kwamba kitatoa maelezo kuhusiana na hatua zaidi zitakazochukuliwa kuelekea Oktoba ni jambo linalitia wasiwasi na hofu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here