Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuendelea kusimamia mpango mkakati wake wa kuwataka wakaazi katika eneo la Kilimani Kisiwani Unguja kuhama ili kupisha ujenzi mpya.
Kadhalika CCM kimewashauri Wakaazi wote wanaoishi kwenye Maghorofa hayo, kukubaliana na uamuzi wa SMZ, unaowataka kupisha Ujenzi wa Mradi wa Nyumba za kisasa.
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema hakuna Serikali inayowaombea wananchi wake wakumbwe na majanga .
Mbeto alisema, kwa muda mrefu SMZ imekuwa akiwashauri Wakaazi wa eneo la Kilimani ambalo lipo karibu na ufukwe wa Bahari, kuhama ili kuupisha ujenzi wa Mradi wa Mji mpya.
Alisema, Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ilipendekeza mpango madhubuti uitwao Dkt. Mwinyi Smart City, lakini ghafla yakazuka mabishano yenye upotoshaji uliovunja dhamira njema.
“Hakuna Serikali yoyote duniani inayowatakia maafa au mabaya Wananchi wake. Eneo la Ardhi la Kilimani linakabiliwa na Mmong’onyoko mkali wa Ardhi. Hakuna njia mbadala zaidi ya kubomoa Nyumba Kongwe na kujenga majengo mapya ya kisasa,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi ,alisema licha ya juhudi za awali za SMZ, kuwataka Wakaazi wa eneo hilo kuhama kwa hiari, waligoma kwa kusikiliza maneno yenye kuwavunja nguvu na ushabiki wa kisiasa.
“Tumepokea taarifa za kuporomoka kwa baadhi ya Nyumba za Kilimani. Nyumba zile zilikuwa kongwe na si salama kwa Makaazi
ya binadamu. Tunaielekeza SMZ iendeleee na mkakati wake wa kujenga Mji mpya wa kisasa ,”alieleza.
Mbeto aliwataka wakaazi wa maeneo hayo kuutafakari ule usemi wa Kiswahili, usemao akili za kuambiwa changanya na zako, hivyo ni lazima wakaazi hao watii na kukubaliana na mpango wa Serikali wa Ujenzi mpya.
“Tutaishangaza dunia ikiwa Wananchi Wakazi wa maeneo hayo wataendelea kukaidi na kutaka kuishi katika majengo hatarishi. Serikali isikubali kusubiri hadi maafa yatokee,” alisisitiza.
Mbeto alisema, mara baada ya Ujenzi huo kukamilika chini ya viwango bora, salama na madhubuti, wananachi waliokuwa na nyumba zao watapewa nyumba mpya huku Serikali chini ya mradi huo ikipangisha nyumba zake.
‘Tuiamini nia njema alionayo Rais Dk Mwinyi na Serikali yake. Ushindani wa Kisiasa usiingilie na kutaka kuvuruga Usalama wa maisha ya watu. Nia na Sera za CCM ni kuiona Zanzibar ikisongambele ,” alisema Mbeto.