π π¨ππππ ππππ ππ πππππππππππ πππ ππ ππ π©πππππππ πππππππππππ ππππ πππππ.
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameelekeza wananchi wa maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo, lakini bado yana mazingira ya vijijini, waendelee kuunganishiwa umeme kwa gharama ya Sh. 27,000, akisisitiza kuwa mabadiliko ya hadhi hayamaanishi kuongezeka kwa uwezo wao wa kiuchumi.
Ametoa maelekezo hayo Oktoba 16, 2026, alipozungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja.
Amesema baadhi ya maeneo yanapotangazwa kuwa miji midogo, wananchi wake huchukuliwa kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha, ilhali hali zao za maisha bado ni za vijijini. Ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuzingatia hali hiyo katika kuwaunganishia huduma.
βWananchi hawa wanaoitwa mji mdogo niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini,β amesema.
Kuhusu hadhi ya Bagamoyo, Dkt. Mwigulu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya kuirasimisha itapatikana wiki ijayo, akisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kinachobaki ni kukamilisha taratibu.
βMheshimiwa Rais tayari alishakwisha kufanya uamuzi, na mimi niwahakikishie mwezi huu huu, wiki ijayo, mtakuwa mmeshapata hati hiyo,β amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Kamishna wa Ardhi kuongoza mwenyewe kliniki ya kusikiliza na kushughulikia kero za ardhi za wananchi wa Bagamoyo kuanzia Jumatatu ijayo.
Ameelekeza afike na timu kutoka makao makuu, ikishirikiana na wataalamu wa mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu β Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kufanya kazi wiki nzima.
βUsitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe,β amesema.