Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema, mgombea wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi amefanya mambo makubwa ya maendeleo, hivyo hana mpinzani kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
Hayo yamesemwa jana Septemba 29, 2025 na Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, kwenye mkutano na wafanyabiashara na wajasiriamali wa soko la Kibandamaiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, ukiwa ni mwendelezo wa mikutano ya Dkt. Mwinyi na makundi mbalimbali.
Mbeto alisema, Dkt. Mwinyi amekuwa muungwana na ameifanyia Zanzibar mambo ambayo hakuna asiyeyaona na kwa hilo, Mungu atamlipa kwani malipo ya wema ni wema, “unachotufanyia Wazanzibari ni wema wa kupitiliza. Wewe umekuwa shuhuda na kinara wa maendeleo.”
Aidha, Mbeto alisema, hivi karibuni akiwa kwenye Jimbo la Konde, wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba alipokwenda kwenye uzinduzi wa kampeni, wazee walimpa ujumbe wa kumfikishia Rais Mwinyi kwa ajili ya kumshukuru kwa mambo yote aliyowafanyia.
Mwenezi alisema, wazee hao wanakiri kwamba, hakuna jambo ambalo Dkt. Mwinyi hajawafanyia; kawajengea shule tatu za kisasa, wana kituo cha afya, kawajengea barabara huku huduma ya maji ikiwa ya uhakika “maji yapo na ziada.”
Mbali na hayo, Mbeto alisema Wazee hao wa Konde walimweleza wana boti zaidi ya 280, huku wakipokea posho yao kupitia Pensheni Jamii “kwa kweli Mheshimiwa Rais umetenda na umeacha alama kama ulivyo msimamo wako.”