Mbeto: Demokrasia ndani ya CCM imechangia wagombea wengi kujitokeza

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

KUWEPO kwa demokrasia katika Chama cha Mapinduzi (CCM), kunatajwa kuchangia ongezeko la wanachama wanaojitokeza kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kukiwakilisha kwenye Ubunge, Udiwani na Wawakilishi katika Uchaguzi Mkuu ujao, Oktoba 2025.

Akizungumza na wanahabari, leo Juni 30, 2025, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema CCM ni chama kikubwa na kinaungwa mkono na makundi yote katika jamii.

Alisema, pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watu wa makundi yote wamejitokeza kuchukua fomu wakiwemo mamalishe, wasanii, boda boda na watu wengine hali inayoonyesha kuwa kinakubalika.

“Nawapongeza kwa mwitikio mkubwa kiasi hicho ingawa tulitarajia kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mwenyekiti Dkt. Samia na Makamu wake, Dkt. Mwinyi inafanya wananchi waone CCM ni sehemu salama,” alisema Mbeto.

Ametaka wanachama zaidi kujitokeza kuomba ridhaa ya chama kwani ndani ya CCM kuna fursa nyingi kuliko upinzani na hakuna mwenye hatimiliki ya uongozi, chama kinaangalia uwezo wa mtu bila kujali iwapo ni tajiri au maskini.

Pia, amebainisha kuwa chama hicho kimeonyesha jinsi gani kinavyokubalika kwa vitendo kutokana na kutii maagizo ya chama ya kuwataka watia nia kwenda kwa utulivu kuchukua na kurudisha bila mbwembwe wala shamra shamra.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here