Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina matumaini na imani kubwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo ipo chini ya Umoja wa Kitaifa.
Vile vile, CCM kimewataka Mawaziri toka CCM na ACT, kuthamini uteuzi na kulinda heshima waliopewa na Rais wa Zanzibar Dkk. Hussein Ali Mwinyi.
Tamko hilo limetamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, akiwa Afisini kwake Kisiwandui Kisiwani Unguja.
Mbeto alisema, Mawaziri na Manaibu wote wana jukumu la kulinda heshima waliopewa na Rais ya kuitumikia Serikali na wananchi kwa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Alisema, baada ya uteuzi wa Mawaziri na Manaibu wake, kazi iliobaki katika kila Wizara, ni kumsaidia kazi Rais ili afanikishe malengo ya kisera ya Serikali kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi .
“Tunampongeza kwa dhati Rais Dkt. Mwinyi kwa uteuzi na mabadiliko madogo katika Baraza lake .Kuna Mawaziri na Manaibu toka CCM na ACT. Tunachowahimiza wakawatumikie Wananchi wote,” alisema Mbeto.
Akielezea zaidi, Katibu huyo Mwenezi alisema kila Waziri ana dhamana na wajibu wa kupigania maslahi ya Umma na kuitumikia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa utii, uzalendo na uaminifu mkubwa.
“Utaratibu mzima wa kuendesha Serikali unafahamika.Kila Waziri dhamana ana wajibu wa kutekeleza majukumu ya kisera. Macho ya Wazanzibari yanawatazama wao,” alieleza.
Mbeto alisema, huu ni wakati wa kuithibitisha dunia kuwa tashwishi za kisiasa, zinaweza kuwekwa kando na maisha yakaendelea bila mivutano.
“Twendeni tukajenge nchi. Maendeleo yanapotokea hayana alama za CCM au ACT. Itapendeza mawaziri wetu wakimudu kutenganisha Siasa na shime ya Maendeleo,” alisisitiza Mwenezi huyo.
Akizungunzia kwa undani, Mbeto alisema maendeleo ya nchi hayana alama ya siasa wala kiitikadi, badala yake maendeleo ya kisekta yakishamiri hunufaisha watu wote.