Na Mwandishi wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitaacha kuzihimiza Serikali zake zizidishe mkazo na kuhakikisha hakuna mtu au kikundi chochote kinachoweza kuvuruga Amani na Umoja.
Vile vile, chama hicho kimefichua siri ya kupatikana kwa maendeleo ya haraka katika Awamu ya Nane Zanzibar; ni kuwepo kwa ustawi wa Amani na Utulivu.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, aliyesema nchi ikiwa katika mazingira ya Umoja, milango ya neema ya Maendeleo hufunguka.
Mbeto alisema, inapokosekana Amani Mshikamano na Utulivu, Serikali haiwezi kujenga miradi mikubwa kama ya Madaraja, Maji, Shule, Barabara, Bandari, Viwanja vya Ndege, Michezo na Masoko.
Alisema, kwa muktadha huo, CCM imekuwa ikizielekeza mara zote Serikali zake zihakikishe hachekewi mtu yeyote atakaethubutu kuvuruga tunu za Amani na Umoja wa Kitaifa.
Pia, Mbeto alitaja kufanikiwa kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo, kumechochewa zaidi na kasi ya ukusanyaji Mapato kwa umakini kulikofanikisha kujenga miradi yenye tija.
“Serikali ya CCM Awamu ya Nane Zanzibar imejitahidi mno kukusanya mapato. Si hivyo tu, lakini pia imesimamia nidhamu ya matumizi ya fedha. SMZ sasa inakopesheka mahali kuliko wakati wowote,” alieleza.
Hata hivyo, katika maelezo yake Mbeto alisema, SMZ hivi sasa ina kibali cha uaminifu wa kukopa katika taasisi zozote za fedha na kwenye benki zote.
“Tunaingia kwenye mbio za Uchaguzi huu tukiwa na mategemeo makubwa ya kushinda. Mgombea wetu Rais Dkt. Mwinyi ni kiongozi mchapakazi, muaminifu na mzalendo,” alisema.
Katibu huyo Mwenezi aliwahakikishia wananchi kuwa ushindi utakaopatikana katika ngwe ya pili, utazidi kutanua wigo wa maendeleo yatakayowashangaza wengi Afrika Mashariki.