Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa hila zinazotumiwa na kundi la Wawakilishi wa ACT Wazalendo, kumchafua Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuhusiana na fidia kwa watu ambao ardhi zao zimechukuliwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazitofanikiwa kwani hakuna ambaye hatalipwa na hana nia ya kumdhulumu Mzanzibari yeyote.
Akizungumza na wanahabari Ofisi Kuu, CCM Kisiwandui, Unguja Septemba 25, 2026, kuhusiana na video inayosambaa ikiwaonyesha baadhi ya wakazi wa Bumbwini na Mangapwani wakidai kuporwa adhi bila fidia, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema Rais Dkt. Mwinyi hajafanya, hatofanya na haitatokea kitu kama hicho.
“Rais Mwinyi ni muungwana sana, hajawahi kufanya na hatafanya yeye na serikali yake kumdhulumu Mzanzibari yeyote haki yake, iwe ardhi, nyumba wala shamba nankila mwenye stahiki yake atalipwa,” alisema Komredi Mbeto.
Alibainisha kuwa, kikundi hicho cha Wawakilishi kimekwenda kinyume na utaratibu kwani hiyo ilipaswa iwe ziara ya kamati ya Baraza la Wawakilishi au wawe wameenda kwa idhini ya Spika wa Baraza la Wawakilishi au vinginevyo iwe Mwakilishi jimboni kwake.
Ufafanuzi huo umetokana na video iliyotengenezwa na kikundi cha Wawakilishi wa ACT Wazalendo na kusambazwa mitandaoni ikiwaonyesha baadhi ya wakazi wa Bumbwini na Mangapwani wakilalamika kudhulumiwa ardhi zao huku wakidai kuna ambao wamelipwa fidia nzuri lakini wao wanadai wamedhulumiwa.
“Serikali hii haijawahi kumdhulumu mwananchi na haitatokea ikafanya vitendo hivyo kwani ni muungwana na kwingineko fidia zimelipwa hadi kwa watu waliovamia maeneo ya Serikali” alisema Komredi Mbeto.
Mwenezi huyo alitanabaisha kuwa propaganda za ACT Wazalendo na kejeli dhidi ya Rais Dkt. Mwinyi kupitia wawakilishi wao hao na kila njia wanazozitumia haziwezi kufanikiwa kwani ukweli upo wazi na kila Mzanzibari aliyeguswa na mradi wowote wa maendeleo amenufaika na fidia na hakuna ambaye hatalipwa.