Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani nchini katika ziara iliyolenga kuzungumzia masuala mbalimbali katika shughuli za uchimbaji na maendeleo ya Sekta ya Madini, Mji wa Serikali jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Septemba 7, 2023, Katibu Mkuu Mahimbali amesisitiza kuimarisha ushirikiano katika uchimbaji wa madini hususan ya kimkakati, kujengewa uwezo wataalam mbalimbali wa Sekta ya Madini ili mnyororo mzima wa shughuli za madini unufaike.
Alisema, Wizara ya Madini imeweka vipaumbele katika maeneo manne ili kuimarisha zaidi Sekta hiyo, maeneo hayo ni pamoja na Utafiti wa kina, maendeleo ya rasilimali watu, ushirikiano sambamba na KanziData ya Madini.
Aidha, amesisitiza kuwa milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini ipo wazi kwa nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye kipaumbele ili nchi zote zinufaike na uwepo wa madini hayo.
Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Kiuchumi kutoka Ubalozi wa Marekani nchini, Jonathan Howard amesisitiza kuwa, nchi yake itashirikiana na Tanzania katika shughuli za Sekta ya Madini hususan katika kujengeana uwezo na ujuzi, fedha na teknolojia.
Vile vile, Howard ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kumteua na kumuapishwa Antony Mavunde kuwa Waziri wa Madini. Wamesema nchi yao itampatia ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kuiongoza Sekta ya Madini.
Aliongeza kuwa, wanatarajia kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Madini linalotarajiwa kufanyika Oktoba 25 na 26, 2023 jijini Dar es Salaam.
Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuvutia wawekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi inayochochea maendeleo na uchumi kwa ujumla..