Mapigano ya wakulima na wafugaji yasababisha vifo Nigeria

0

MAIDUGURI, Nigeria

MAPIGANO kati ya wafugaji na wakulima yaliyotokea katika Jimbo la Benue la Kaskazini mwa Nigeria yamesababisha vifo vya watu 23.

Paul Hembah, mshauri wa masuala ya kiusalama wa gavana wa Jimbo la Benue, ameliambia shirika la habari la ‘Anadolu’ kuwa mapigano yalianza kufuatia uvamizi wa jamii ya wakulima ya Gbeji katika wilaya ya Ukum kulikofuatiwa na mapigano ya risasi siku ya Jumatano.

Alisema, mbali na kuuawa watu hao 23, wanakijiji wengine wengi wamejeruhiwa katika mapigano ya takriban masaa mawili ya kugombania malisho na mashamba ya kilimo.

“Tumepata maiti zaidi. Waliothibitishwa hadi sasa ni 23 na bila shaka wahanga wa mapigano hayo wanaweza kuongezeka kadiri tunavyoendelea kuwatafuta vichakani.” alisema.

Polisi na wanajeshi wamefika eneo la tukio ili kuzuia mapigano hayo yasisambae kwa jamii jirani.

“Mgogoro ulianza Jumanne wakati wafugaji watano wa kabila la Fulani walipovamiwa na kuuawa katika matukio matatu tofauti na mifugo yao kuibiwa,” alisema Kamishna wa Polisi wa Benue, Wale Abbas.

Mwaka 2021 Jimbo la Benue la kaskazini-kati mwa Nigeria lilipitisha sheria ambayo inakataza malisho ya wanyama katika maeneo ya wazi.

Mapigano kuhusu malisho ya wanyama na matumizi ya maji yanatokea mara kwa mara katika majimbo ya kaskazini mwa Nigeria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here