Majaliwa awataka wadau kuchangia utatuzi wa changamoto kwenye sekta ya afya

0

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya iendelee kuhamasisha taasisi, na wadau kuchangia maeneo muhimu kama ya afya hasa yanayogusa jamii ikiwemo fistula, na saratani ambayo yanasumbua jamii.

“Suala la kuchangia maendeleo na utatuzi wa changamoto za jamii ni la Watanzania wote. Kwa umoja wetu tukishirikiana, tutaifanya Tanzania yetu kuwa salama zaidi. Hivyo, nitoe rai kwa makampuni mengine yanayofanya biashara hapa nchini kushirikiana na Serikali ili kwa pamoja tutatue changamoto hizo,” amesema.

Akizungumza na mamia ya washiriki wa mbio za hisani za NMB leo kwenye viwanja vya Leaders’ Club jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema, Serikali pamoja na jitihada zake za kutoa huduma, bado inahitaji kuungwa mkono na Watanzania na yeyote ambaye ameguswa na jambo hilo ili kunusuru maisha ya mama zetu.

“Taarifa za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa akinamama wengi, wanasumbuliwa na tatizo la fistula lakini wengi wao wamepoteza matumaini kwa sababu hawawezi kumudu gharama za matibabu. Hivyo, wanapotokea watu wa kuwasaidia, hatutasita kushirikiana nao ili kuhakikisha mama zetu, dada zetu na hata watoto wetu wanapata msaada,” alisema.

Ameipongeza benki ya NMB kwa kufanikiwa kuchangisha Shilingi Bilioni moja ndani ya miaka miwili badala ya miaka minne kama iliyopangwa awali. “Utaratibu kama huu wa benki ya NMB kusaidia jamii ambao umeonesha mafanikio makubwa ya kuchangia Shilingi bilioni moja kwa miaka miwili tu, ni wa kuigwa na taasisi nyingine. Mwaka jana tulipata shilingi milioni 400 badala ya Shilingi Milioni 250 zilizokusudiwa. Mwaka huu tumepata Shilingi Milioni 600 badala ya Milioni 250.”

Amezipongeza kampuni za bima za Sanlam kwa kuchangia sh. milioni 150 na kampuni ya bima ya UAP kwa kuchangia Shilingi Milioni 100. Mbio hizo zilianzia kwenye viwanja vya Leaders’ jijini Dar na kuzunguka viunga vya jiji la Dar na kuishia kwenye viwanja hivyo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Michezo Nchini (BMT) lisimamie mashirikisho ya michezo yote kuandaa mipango itakayojumuisha watu wengi kushiriki michezo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Pia, amekiagiza Chama cha Riadha Tanzania (RT) kiendelee kuhakikisha mbio nyingi zinazofanyika nchini zinaratibiwa vizuri na kuhamasisha jamii kushiriki. Pia, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kusajili vikundi mbalimbali vya riadha, jogging na aina nyingine ya mazoezi.

“Manispaa za Temeke, Kinondoni, Ilala na nyinginezo, ziwatambue rasmi wanaoshiriki kwenye hivi vikundi na kuwasaidia kutambuliwa kwa shughuli zao kwa sababu vinasaidia kukuza hamasa ya michezo katika jamii,” alisisitiza.

Pia, ameyataka mashirika, makampuni na majeshi nchini yarudishe utaratibu wa kuunda vikundi vya kuibua vipaji ili kurudisha hadhi ya nchi katika mashindano ya Kimataifa.

Mapema, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema benki yao imeandaa mbio hizo za hisani za marathon (Mwendo wa Upendo) ili kuchangia matibabu ya wanawake wenye tatizo la fistula. Alisema mwaka jana waliweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni moja kwa kipindi cha miaka minne lakini wamelitimiza ndani ya miaka miwili.

“Takwimu zilizopo zinaonesha wanawake 10,000 wana fistula na kila mwaka wanaongezeka 3,000 lakini wanaopata matibabu ni 1,300. Na gharama ya kumtibu kila mmoja ni Shilingi Milioni nne. Kwa hiyo, fedha zilizokusanywa zitatumika kulipia matibabu ya wanawake 250,” alisema.

Viongozi walioshiriki mbio hizo ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuberi Ali Maulid, Naibu Spika, Mussa Azzan Zungu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Shaka Hamdu Shaka, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Godwin Gondwe, Mameya wa Dar es Salaam na Zanzibar, Wabunge wa Ukonga na Kibamba, wakurugenzi wa taasisi na mashirika mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here