Maambukizi ya VVU yapungua Ruvuma

0

Na Angela Msimbira, RUVUMA

MKUU wa Mkoa wao Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema, maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI yamepungua kwa asilimia 0.7 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 mwaka 2022 Mkoani Ruvuma.

Ameyasema hayo wakati akifungua wiki ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani humo.

Kanali Abbas alisema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya watu 68,237 wanaoishi na VVU ambapo wanaume ni 24,959 sawa na asilimia 37 na wanawake ni 43,000 sawa na asilimia 63 huku watoto chini ya miaka 15 ni 2382 sawa na asilimia 3.5.

“Halmashauri zinazoongoza ni Manispaa ya Songea ikifuatiwa na Tunduru na Mbinga hivyo nawasihi watu wanao ishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) wote kuzingatia tiba na matunzo ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza virusi ikiwa ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huu,” alisema Kanali Abbas.

Aidha, ametaja vichocheo vinavyosababisha maambukizi mapya kuwa ni pamoja na mwingiliano wa watu na shughuli za kiuchumi hivyo amewataka wananchi kujikinga ili wasipate maambukizi.

Naye, Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim ameupongeza Mkoa wa Ruvuma kwa mapambano ya kushusha kiwango cha maambukizi ikiwa ni pamoja na kuongoza kwa upimaji wa virusi vya UKIMWI kitaifa.

“Mkoa wa Ruvuma umeendelea kufanya vizuri katika viwango vya “95 95 95” ambapo utafiti wa mwaka 2023 unaonesha asilimia 82 za wananchi wa mkoa huo wanatambua hali zao za maambukizi na asilimia 97 wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na asilimia 90 ya wanaotumia dawa wameshafubaza virusi hivyo”, alieleza Dkt. Catherine.

Wiki ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yanafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ambapo kitaifa yanafanyika Mkoani Ruvuma na yanatarajiwa kufungwa Desemba 1, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here