LATRA waagizwa kutoa huduma Saa 24

0
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa Malekezo kwa Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Mwanza, Halima Lutavi, wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka hiyo jijini Mwanza.

Na Jumbe Abdallah

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Nchini (LATRA), kupitia Kitengo cha Huduma kwa Wateja kufanya kazi saa 24 ili kutatua kwa wakati changamoto za wasafirishaji.

Naibu Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo jijini Mwanza mara baada kukagua shughuli za udhibiti usafiri wa ardhini na kubaini uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo utoaji wa vibali vya safari na utoaji wa stika.

“Wasafirishaji hawa ni wafanyabiashara akichelewa masaa mawili au matatu tayari amepoteza fedha nyingi na hili ninyi ndio mnasababisha kwa kuchelewesha kuwapa vibali na stika, jipangeni vizuri kuanzia mkoa mpaka makao Makuu ili malalamiko haya yaishe”, alisema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameitaka LATRA kukaa na Jeshi la Polisi Nchini ili kufanya kaguzi za kushtukiza na kupanga mikakati inayotekelezeka itakayopunguza ajali nchini kwasababu ajali zimeendelea kuongezeka na kupoteza nguvu kazi ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Mwanza, Halima Lutavi, ameeleza kuwa changamoto ya vibali mfumo unapokuwa na shida LATRA huwasiliana na Jeshi la Polisi ili kuwaruhusu wasafirishaji kuendelea na safari ili kutowachelewesha.

Mfawidhi Halima aliongeza kuwa, kwa sasa Mamlaka inaweka mikakati ya kuboresha usafiri wa pikipiki na bajaji kwa kutengeneza njia maalum ili kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa usafiri huo katika miji.

Naibu Waziri Mwakibete yuko Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili kukagua miradi ya maendeleo na kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Sekta ya Uchukuzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here