Kwa ubaguzi wa Jussa, hakuna aliye salama

0

Na Mwandishi Wetu

KWA siku za karibuni, nimesoma maandiko kadhaa yanayomkosoa na kumkemea Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Ismail Jussa Ladhu na kauli zake za kibaguzi anazozitoa kwa lengo la kutaka kuwagawa Wazanzibar.

Kauli za Jussa pia zina lengo la kutaka kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka mingi na umekuwa mfano wa kuigwa, huku ukiendelea kuimarika tangu ulipoasisiwa Aprili 26, 1964 na viongozi wetu Sheikh Abeid Aman Karume na Mwalimu Julius Nyerere.

Jussa amekuwa akitoa kauli za kibaguzi kwa watu kutoka Bara, watu wa dini tofauti na yake, vile vile amekuwa akimbagua kila mwenye ‘rangi nyeusi’ bila kujali ni mzaliwa wa Unguja au Pemba, na kwa mujibu wa watu wake wa karibu, wanadai amekuwa akitamka wazi kwamba, ‘watu weusi Visiwani sio kwao.’

Kwamba, Zanzibar ni nchi ya Waarabu, ndio maana licha ya kuwa na asili ya Asia, lakini yeye na kikundi cha wabaguzi wenzake wachache, wamekuwa wakijiita ni watu wa Oman wanaoishi Zanzibar.

Ni Jussa na wenzake ambao wamewahi kumbagua Makamu wa Rais wa Awamu ya Tatu, Marehemu Dkt. Omari Juma, pia miaka ya karibuni walimbagua aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Idd na wamekuwa wakiwabagua wote ambao wanaona ‘sio waraabu wenzao.’

Ubaguzi wa Jussa haujaishia hapo, wakati wa bunge Maalum la Katiba, amewahi kumbagua mmoja wa wajumbe Amon Mpanju, ambaye ni mlemavu wa macho, ambapo wakati akichangia, aliomba kumpa taarifa.

Mpanju baada ya kumaliza kutoa taarifa yake, Spika alimuuliza Jussa kama anaikubali, lakini katika hali ya kushangaza, alijibu: “Naipuuza taarifa ya Mpanju kama ninavyompuuza yeye mwenyewe.”

Kauli hiyo ilikemewa na kupingwa na watu wengi, ilitarajiwa Jussa angefafanua kauli yake au kuomba radhi, lakini kwasababu ya kiburi alichonacho na jinsi alivyotawaliwa na roho ya ubaguzi, alikaa kimya hadi leo.

Kwa maana hiyo, ikatafsiriwa anampuuza Mpanju kwa sababu ya ulemavu wake ambao hakuomba azaliwe hivyo ili aje duniani kupuuzwa na watu kama Jussa ambaye anaamini hawezi kupata ulemavu.

Jussa kwa kiburi alichonacho, hataki kusikia maneno ya wahenga kwamba ‘kabla hujafa hujaumbika,’ wala hana habari na yanayosemwa kwamba kila mmoja ni mlemavu mtarajiwa na kwamba kwake ukiwa mlemavu kama alivyo Mpanju, hauna cha kumshauri na atakupuuza.

Kama vile haitoshi, Jussa kwa kiburi alichonacho, amewahi kuwazuia watu wa Bara kuzungumza masuala yanayohusu Zanzibar, kana kwamba yeye ndiye mwenye Mamlaka ya kuongoza visiwani hivyo na kuamua nani aongee na nani asiongee!.

Huyo ndiye Ismail Jussa Ladhu ambaye watu wanadhani kauli zake anazitoa kwa bahati mbaya; wanapaswa kujua kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo anakusudia, ubaguzi ni tabia yake.

Kama kipo kikundi au watu wachache ambao wanashabikia anayoyafanya, au wanaamini hayawahusu, watambue kwa haya anayoyafanya, hakuna aliye salama. Jussa anapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here