Kujiua kwa askari, ni mfupa uliowashinda Marekani?

0

WASHNGTON, Marekani

IDADI ya askari wanaojiua katika Jeshi la Marekani imezidi kuongezeka mwaka uliopita wa 2021 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa askari 176 walijiua.

Kwa mujibu wa ‘Pars Today’ takwimu hizo za Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, zinaonyesha kuwa, jeshi hilo limekuwa likijaribu kutafuta njia za kuimarisha kiwango cha maisha ya askari ili kuboresha afya yao ya kiakili.

Tovuti ya military.com pia imeandika kuwa kuna idadi kubwa ya askari wanaojiua katika Gadi ya Kitaifa ya Marekani ambapo maafisa 102 wa kikosi hicho walijiua mwaka 2021. Aidha, Gadi ya Kitaifa ya Anga ilitangaza maafisa wake 15 walijiua mwaka jana.

Hayo yanajiri wakati ambao takwimu mpya zinaonyesha kuna ongezeko kubwa la hujuma za kijinsia katika Jeshi la Marekani ambapo mwaka 2021 kuliripotiwa ongezeko la asilimia 25.6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Mwaka jana, utafiti mpya ulifichua kuwa, idadi ya askari wa Marekani na Maveterani wa jeshi wa nchi hiyo wanaoaga dunia kwa kujitoa uhai ni mara nne zaidi ya wanajeshi wanaouawa vitani tokea Septemba 11 mwaka 2001.

Inaonekana kuwa, suala hilo la kujiua kwa wingi wanajeshi wa Marekani hususan wale walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq ni miongoni mwa matunda ya vita visivyo na ukomo vya watawala wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya dunia kwenye miongo miwili iliyopita.

Mbali na hayo, maelfu ya wanajeshi wa Marekani walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq na kuendeleza uvamizi wa Washington katika nchi hizo wanasumbuliwa na aina mbalimbali za matatizo na magonjwa ya kiakili na kinafsi.

Inaelezwa, askari hao wanaporejea makwao huonekana kuwa na mienendo ya ajabu na isiyofaa kwa watu wa familia zao na katika jamii na hatimaye huamua kujitoa uhai kwa kujiua wenyewe baada ya kushindwa kustahamili adhabu na matatizo mengi ya kinafsi na kiakili.

Mwaka 2021, Wizara ya Ulinzi nchini Marekani (Pentagon) ilitahadharisha juu ya ongezeko la kujiua maafisa wa jeshi la anga la nchi hiyo, ambapo taarifa ya Wizara hiyo ilionyesha kuwa, kuna ongezeko kubwa la askari kujiua.

Aidha, viongozi wa jeshi la anga walitangaza kuwa kiwango cha kujiua ndani ya jeshi hilo kiliongezeka kwa asilimia 33 mwaka 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Jeshi la anga la Marekani pia limeongeza kuwa jumla ya askari 137 wanaohudumu katika jeshi la anga na ambao ni walinzi wa taifa na akiba ya jeshi la anga walijiua mwaka jana, ambapo uongozi wa kitengo hicho ulikiri wazi kwamba, sio rahisi kufahamu njia za kukabiliana na ongezeko la kujiua kwa askari hao.

Taarifa nyingine zinadai kwamba, kuna uwezekano mkubwa wanajeshi wote wa Marekani ambao walishiriki mstari wa mbele wa vita mbalimbali wakapatwa na aina mojawapo ya matatizo ya kinafsi na kiroho hadi mwishoni mwa umri wao.

Vifo vinavyotokana na kujiua wanajeshi wa Marekani mbali na kuangamiza familia zao, lakini pia vinasambaratisha moyo na mshikamano wa ndani ya vikosi vya majeshi walivyokuwa wakitumikia.

Uchunguzi uliofanyika kuhusu visa hivi vya kujitoa roho wanajeshi wa Marekani unaonesha kwamba, wanajeshi hao waliwahi kuwa katika maeneo ya vita, kukumbwa na sonono, matatizo ya kinafsi, utumiaji mbaya wa dawa na matatizo ya kibinafsi.

Baadhi ya wataalamu wa elimu nafsi pia wanasema, ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Marekani katika maeneo kama Afghanistan na Iraq na mienendo mibaya ya maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani dhidi ya wale walioko chini yao na kadhalika vimezidisha msongo wa mawazo na mashinikizo ya kinafsi ya wanajeshi hao na hatimaye kujiua wenyewe.

Vilevile Maveterani wengi wa Marekani wanasumbuliwa na hali mbaya ya kimaisha ambayo mara nyingi huwasukuma upande wa kujitoa uhai.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here