Jinsi Qatar inavyotumia ardhi na bahari kiuchumi

0

Na Fowad Mehd

KATIKA ardhi ya Qatar, kilimo kinachukua nafasi ndogo kwa sababu ya ukame na ardhi isiyofaa kwa kilimo. Lakini, kabla ya karne ya 20, kilimo cha wakulima wadogo wadogo, ufugaji wa kuhama hama na uvuvi ndizo zilikuwa njia kuu za uchumi wa wananchi.

Shughuli za baharini kama uvunaji wa lulu na samaki zilitumika kama vyanzo vikuu vya mapato vya Waqatari hadi pale nchi ilipoanza uchimbaji wa mafuta mwaka 1939.

MASHAMBA YA KUMWAGILIA NCHINI QATAR

Ingawaje shughuli hizo za awali zimepungua huku biashara ya lulu ikiwa imetoweka kabisa, bado serikali inafanya jitihada za kuhamasisha kilimo na Uvuvi ili kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula.

HISTORIA

Mitende ndiyo mazao ya awali kabisa kulimwa katika nchi hiyo. Tangu zama za kati, biashara ya tende ilikuwa na athari muhimu katika Uchumi wa Qatar. Miti ya mitende nayo, kwa kawaida, ilitumika kama vifaa vya ujenzi. Uvunaji wa lulu ndio ulikuwa chanzo kikuu cha mapato kwa wananchi wa Qatar hadi yalipovumbuliwa mafuta Karne ya 20. Biashara ya lulu, katika baadhi ya maeneo, iliendana na biashara ya uzalishaji wa ngamia. Uvuvi nao ukachangia Uchumi.

KILIMO NA MIFUGO

Ni asilimia 2.5 (hekta 28,000) ya ardhi ya Qatar ndiyo inayofaa kwa matumizi ya ufugaji. Hili ni ongezeko kubwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Mwaka 1996, hekta 8,312 za ardhi ndizo zilizofaa ilihali mwaka 1980 hekta 256 tu ndizo zilizofaa.

Hivi sasa kilimo kinachangia sehemu ndogo tu ya uchumi wa nchi hiyo. Kati ya hekta 8,312 za ardhi ya kufaa kwa kilimo, ni hekta 2,345 tu zilizotumika mwaka 1994 kwa ajili kilimo cha mazao ya kudumu, ilihali hekta 5,987 zilitumika kulima mazao ya msimu. Mitende ndiyo zao kuu la kudumu.

Kati ya mwaka 1960 na 1970, sekta ya kilimo ilizidi kukuwa. Idadi ya mashamba iliongezeka hadi kufikia 411. Waqatari wanaomiliki ardhi ya kilimo, kwa kiasi kikubwa, ni wale wenye kazi serikalini, ambapo ardhi yao huikodisha kwa Wairan na Wapakistan au Warabu ambao si wenyeji wa Qatar ili wayaendeshe mashamba.

Serikali huendesha shamba moja tu la majaribio. Katika ardhi iliyolimwa mwaka 1990, takribani asilimia 48 ilitumika kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga ambapo jumla ya tani 23,000 zilizalishwa.

Asilimia 33 ya ardhi ilitumika kwa ajili ya kilimo cha matunda na tende ambapo tani 8,000 zilizalishwa, asilimia 11 ya ardhi ilitumika kwa ajili ya chakula cha mifugo ambapo tani 70,000 zilizalishwa, na asilimia 8 ya ardhi ilitumika kuzalisha nafaka ambapo tani 3,000 zilizalishwa.

Mwaka 1990, nchi ilikuwa na takribani Kondoo 128,000, Mbuzi 78,000, Ngamia 24,000, Ng’ombe 10,000 na Farasi 1,000. Aidha, kuna mashamba ya ng’ombe wa maziwa, na kuku wapatao 2,000.

Asilimia 20 ya mahitaji ya mayai inatimizwa ndani ya nchi. Licha ya uhamasishaji wa kilimo na uvuvi, maeneo haya mawili ya uchumi kwa pamoja yalichangia asilimia 1 tu ya Pato la Taifa (GDP) mwaka 1989.

UVUNAJI WA LULU

Uvunaji wa lulu ndio ulikuwa chanzo kikuu cha mapato nchini Qatar hadi yalipovumbuliwa mafuta mwaka 1939. Inakadiriwa vichanja 85 vya lulu (pearl beds) vipo katika bahari kuu. Kihistoria, msimu wa mavuno ya lulu uligawanyika katika vipindi vitatu.

Kipindi cha ‘Hansiyah’ kilichoanza katikati ya Mwezi Aprili na kudumu kwa siku 40. Kipindi cha ‘Ghaus Al Kebir,’ kipindi kikuu cha kuzibilia (kupigia mbizi) lulu kilichoanzia Mwezi Mei hadi Septemba 10.

Mwisho, ni kipindi cha ‘Ruddah’ kilichoanzia mwishoni mwa Mwezi Septemba hadi Oktoba. Kuanzia karne ya 18 hadi ya 20, kiasi kikubwa cha lulu zilisafirishwa kwenda Mumbai ambako ziliainishwa na kupelekwa kwenye masoko ya Ulaya. Mavuno yaliyosalia yalipelekwa kwenye masoko ya Baghdad.

UZAMIAJI WA LULU KATIKA GHUBA YA UAJEMI

Chaza ya Zubara Kaskazini Magharibi mwa Pwani ya Qatar ni moja ya chaza za lulu zilizohifadhi na zenye eneo kubwa katika ukanda wa bahari wa nchi hiyo. Kukifikia kilele chake katika karne ya 18 ndiko kulikoiwezesha Qatar kuwa na bandari kubwa na kituo kikubwa katika njia za Ghuba. Baada ya kuingizwa kwa lulu za kuchonga katika karne ya 20, uvunaji wa lulu ukasita kuwa njia mbadala ya uchumi kwa Waqatari wengi.

UVUVI

Kampuni ya Uvuvi ya Taifa, ‘Qatar National Fishing Company,’ ilijumuishwa mwaka 1966 kuvua kamba katika bahari kuu na kisha kuwachakata kiwandani. Japan ndiyo soko kuu la samaki wa biashara wa nchi hii. Uvunaji wa samaki na wanyama wengine wa majini kwa mwaka 1989 ulikuwa ni tani 4,374.

VIKWAZO

Hali ngumu ya hewa kama joto kali kupindukia, ukame na ukosefu wa ardhi yenye rutuba ndiyo inayokwamisha kasi ya uzalishaji wa kilimo. Aina ya udongo unaochukua sehemu kubwa ya nchi ndiyo inayofanya takribani hekta 1,020,000 zisifae kwa kilimo.

Uchache wa maji ya ardhini ambayo ndiyo yanayostawisha kilimo katika baadhi ya maeneo pamoja na maji ya chumvi ndio unaoifanya ardhi isiwe rafiki kwa mazao yote isipokuwa yale yanayohimili chumvi.

Sehemu ya Kaskazini ya Qatar inajumuisha chanzo muhimu cha maji safi ya ardhini, kwa kiasi kikubwa kutokana na jiolojia ya majimaji ambayo ipo zaidi huko kuliko maeneo ya Kusini ya nchi.

Kiasi cha maji ya ardhini kilichovunwa mwaka 1966 kilikuwa ni mililita 20 (20mm3) kwa mwaka. Hii ikaongezeka hadi kufikia mililita 120 (120mm3) mwaka 2000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here