Na Jumbe Abdallah
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariamu Mwinyi amesisitiza umuhimu wa jamii kujikita katika kufanya mazoezi kwa kigezo kuwa hujenga afya, kuleta urafiki, upendo na kushajiisha amani.
Mama Mariamu alisema hayo huko Dole Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja baada ya kukamilisha mazoezi ya viungo, yaliowashirikisha wanamichezo kutoka makundi mbali mbali, ambapo yalitanguliwa na matembezi ya hiari yaliyoanzia Halmashauri ya Wilaya Magharibi ‘A’ Kianga hadi Viwanja vya Dole.
Akizungumza na wanamichezo hao alisema, mazoezi huleta afya na kufafanua kuwa watu wenye afya huwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi, hivyo akatoa wito kwa jamii kufanya mazoezi kila inapopatikana nafasi na kulifanya jambo hilo kuwa sehemu ya maisha yao.
Alisema, kupitia mikusanyiko ya aina hiyo jamii hupata fursa ya kupokea taarifa mbali mbali, ikiwemo changamoto zinazowakabili kwa dhamira ya kuzitafutia ufumbuzi.
Mama Mariamu alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kuchanja katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, akibainisha namna watu kadhaa walivyopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Aidha, alielezea umuhimu wa wazazi na walezi katika kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao pamoja na kufuatilia nyendo zao kwa kigezo kuwa kumekuwa na baadhi ya wanafunzi wanaotoka nyumbani na kuishia njiani wakati wakielekea skuli kwa sababu mbali mbali za utoro.
“Elimu humpa mtu taarifa , maarifa na ustadi pamoja na kusimamia maadili…elimu ni ufunguo uanaofungua fursa mbambali za kimaisha”, alisema.Alieleza kuwa Taifa linahitaji wataalamu katika fani mbali mbali, na kusema elimu ni muhimu katika kufikia malengo hayo.
Nae, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema, Wizara hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Mama Mariamu Mwinyi kupitia Jumuiya yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) katika kuihamasisha jamii kufanya mazoezi.
Mapema, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa aliwashukuru wanamichezo wote walioshiriki mazoezi hayo, ambapo pamoja na mambo mengine alisema, hatua hiyo ni muhimu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kijamii zinazokabili Wilaya hiyo, akitolea mfano wa suala la utoro mashuleni.
Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo Suzan Kunambi, aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito wa kushirki katika mazoezi hayo, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ZMBF na kusisitiza azma ya Ungozi wa Wilaya hiyo kuendelea kuwashajiisha.