Na Mwandishi Wetu
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema, Serikali imeendelea kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo na ruzuku, hatua inayowezesha kupanuka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ufadhili.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia ameyasema hayo Jumatatu, Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambapo aliishukuru Serikali kwa kuzingatia mahitaji na umuhimu wa elimu ya juu na kumekuwa na rekodi ya bajeti na idadi ya wanufaika kupanda mwaka hadi mwaka.
Alisema, katika mwaka wa masomo 2025/2026, HESLB ilitumia Shilingi bilioni 916.7 kuwahudumia wanafunzi 289,932, huku bajeti ya mwaka wa masomo 2026/2027 ikipanda hadi Shilingi Trilioni 1.06, ambapo ongezeko hilo la asilimia 15.6 amesema, linaonesha dhamira ya kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa Watanzania wenye sifa na mahitaji ya kifedha.
Dkt. Kiwia alisema, HESLB ilitangaza awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027 Jumamosi, Oktoba 10, 2026, ambapo jumla ya wanafunzi 165,775 walipangiwa ufadhili wenye thamani ya Shilingi Bilioni 535.7.
Ufadhili huo unahusisha wanafunzi wa shahada ya awali, stashahada, wanafunzi wanaoendelea na masomo pamoja na wanufaika wa programu ya Samia Scholarship waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika kundi la wanafunzi wapya wa shahada ya awali, wanafunzi 74,769 walipangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 246.88. Wengine 8,538 wa ngazi ya stashahada walipangiwa mikopo ya Shilingi Bilioni 22.9 huku wanafunzi 873 wakipangiwa ruzuku ya Shilingi Bilioni 4.5 kupitia Samia Scholarship.
Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, wanafunzi 79,115 walipangiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 252.4.
Aidha, wanafunzi 1,554 wa stashahada walipangiwa mikopo ya Shilingi Bilioni 3.8, huku wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Shilingi Bilioni 5.1.
Dkt. Kiwia alisema, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanaendelea na masomo yao bila kukatizwa na changamoto za kifedha.