DMI wapata mtambo wa Kisasa wa Bilioni Mbili

0
Mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) akifanya mazoezi kwa vitendo kwenye mtambo maalum wa Kidigitali wa kunyakulia mizigo (Crane Simulator) chuoni hapo jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili kununulia mtambo maalum wa Kidigitali wa kunyakulia mizigo (Crane Simulator) ili kurahisisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma kozi za uendeshaji mitambo katika wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Chuo cha DMI Dkt. Tumaini Gurumo alisema, elimu ya uendeshaji wa mitambo unahitaji wahitimu kufanya mazoezi ya nadharia na vitendo ili kuwezesha kuwa mahiri katika utendaji.

“Kozi za uendeshaji wa mitambo hususani kwenye mitambo ya kunyakua vitu vizito zinahitaji uzoefu kwenye nadharia na vitendo hivyo kupitia mtambo huu wanafunzi watatakiwa kufuzu kwenye maeneo yote ili kuwezesha kufanya kazi kwa weledi, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha jambo hili” alisema Dkt. Tumaini.

Dkt. Tumaini alisema, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa chuo cha DMI lengo likiwa kuhakikisha chuo hicho kinazalisha wataalam watakaoweza kushindana sokoni, lakini kwa kuendesha miradi mikubwa inayotekelezwa nchini hasa miradi ya ujenzi wa meli katika maziwa Nchini.

Kwa upande wake Mkufunzi wa DMI, Elinathan Blasius alisema mtambo huo wa kisasa unaotumia teknolojia ya kompyuta utawawezesha wahitimu kwenda na wakati hasa kwenye upakiaji na upakuaji wa mizigo katika bandari, Viwandani na kwenye migodi.

Kwa upande wake Mwalimu Leonard Mwesiga ametoa rai kwa wanafunzi wanaopenda kujiunga na kozi hiyo kutuma maombi ili kuongeza wataalam kwenye eneo la uendeshaji mitambo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here