Dkt. Mwinyi: WanaCCM jivunieni mafanikio yaliyopatikana

0

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa mafanikio ambayo CCM imeyapata ndani ya miaka 48 tangu kuasisiwa kwake ni kielelezo muhimu cha ubora wake na tofauti yake na vyama vingine vya siasa ndani na nje ya nchi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipohutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Februari 5, 2025.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Wana-CCM wana kila sababu ya kujivunia mafanikio hayo kutokana na utekelezaji wa malengo ya chama katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Halikadhalika, Dkt. Mwinyi amewahimiza Wana-CCM kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na hatimaye kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao ili CCM ipate ushindi mkubwa na kuendelea kushika dola.

Kwa upande mwingine, Dkt. Mwinyi amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukiongoza chama hicho kwa umahiri na kuzisimamia Serikali zote mbili katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa miaka 48 iliyopita baada ya kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP Februari 5, 1977, tukio lililofanyika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here