MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inakusudia kujenga nyumba 5,000 za makaazi kwa wananchi wa Unguja na Pemba ndani ya kipindi cha miaka mitano kupitia Shirika la Nyumba la Zanzibar(ZHC).
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Mei 13, 2026, katika mkutano maalum wa kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema Serikali imeweka mkazo katika ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuwaondoa wananchi wanaoishi katika nyumba chakavu na zisizo salama, huku akibainisha kuwa baadhi ya nyumba zilizojengwa zaidi ya miaka 62 baada ya Mapinduzi zinahitaji kufanyiwa maboresho au kujengwa upya.
Aidha, Dkt. Mwinyi amewahimiza wanachama wa CCM kuendelea kuimarisha Chama kwa kudumisha mshikamano, kurejesha madarasa ya itikadi na kuanzisha miradi ya kiuchumi yenye tija katika wilaya na mikoa.
Ziara ya kutoa shukrani kwa wanachama baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 imehitimishwa leo Kisiwani Pemba baada ya kuanza rasmi Mei 9, 2026.