RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini katika kudumisha amani nchini.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe Januari 6, 2026 alipoizindua Ijitimai ya Kimataifa ya kila mwaka inayoandaliwa na Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz, inayofanyika Fuoni Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi pamoja na taasisi za kidini ili kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu, huku akiwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kufahamu kuwa Uislamu unasisitiza elimu, mawaidha na hekima katika maisha ya kila siku.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa jukumu la kuamrisha mema si suala la kuwaachia viongozi wa dini pekee, bali ni jukumu la kila mmoja, na kwamba waumini wana wajibu wa kuhamasishana kutenda mema na kusaidiana.
Amewahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzidisha ibada na kumcha Mwenyezi Mungu, sambamba na kuwataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bei za bidhaa za chakula wakati wa Ramadhani.
Mapema, Alhaj Dkt. Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti huo.
Naye Khatibu wa Msikiti huo, Sheikh Khamis Shaaban, amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kusameheana pale walipokoseana na kuishi kwa kumcha Mwenyezi Mungu.
Ijitimai hiyo ya Kimataifa imehudhuriwa na masheikh pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati.