RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru India kwa kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar katika sekta mbalimbali za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa shukrani hizo leo Mei 14, 2026, alipokutana na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar, Balozi Kumar Praveen, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa kwa ushirikiano wa India umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengi ya mijini Unguja na Pemba.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kupitia mradi mpya wa maji wenye thamani ya takriban dola milioni 35 za Marekani, utakaohusisha uendelezaji wa skim tisa za maji, uwekaji wa matanki mapya, uchimbaji wa visima, ujenzi wa mtandao wa mabomba pamoja na ujenzi wa jengo la afisi ya mradi huo.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesifu mchango wa Chuo cha IIT Madras kilichopo Zanzibar kwa kuendelea kutoa mafunzo na kuleta mageuzi katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Halikadhalika, ameipongeza India kwa kutoa fursa za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wananchi wa Zanzibar katika sekta mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa fursa hizo ili kuongeza uwezo wa rasilimali watu nchini.
Katika sekta ya afya, Rais Dkt. Mwinyi ameomba kuimarishwa zaidi kwa ushirikiano kati ya Zanzibar na taasisi za afya za India kupitia utoaji wa huduma na mafunzo kwa madaktari na watendaji wa afya.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uwekezaji wa taasisi binafsi za India katika miradi ya nishati mbadala Zanzibar, akieleza kuwa uwekezaji huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kuwa na umeme wa uhakika na kujitegemea.
Kwa upande wake, Balozi Kumar Praveen ameihakikishia Zanzibar kuwa India itaendelea kuimarisha ushirikiano wake, huku akisifu kasi ya maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii inayotekelezwa Zanzibar, ikiwemo barabara na viwanja vya ndege.