DART watakiwa kudhibiti upotevu wa Mapato

0

Na Angela Msimbira OR- TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki amewaagiza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha inadhibiti uvujaji wa mapato kwa kuweka mifumo mizuri inayoweza kuzuia tatizo hilo.

Ametoa rai hiyo Oktoba 12, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu, karakana na maeneo mengine yaliyo chini ya DART, jijini Dar es Salaam na kuupongeza Wakala huo kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa za kudhibiti mapato na kuutaka kuongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha mapato ya Serikali hayapotei

“Hakikisheni mifumo yenu ni salama hakuna mianya ya upotevu wa mapato na hakikisheni mifumo inakaguliwa ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato kwenye vituo vya kukatia tiketi,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Alisema, kwenye TEHAMA kumekuwa na changamoto nyingi, hivyo amewaelekeza kufanya ukaguzi na mapitio ya mara kwa mara ya mifumo kwa lengo la kujiridhisha kwenye suala la ukusanyaji wa mapato.

Pamoja na hilo pia Waziri Kairuki ametoa onyo kali kwa wananchi wote wanaoingilia miundombinu ya Mabasi hayo yaendayo haraka huku akisisitiza kuwa kuanzia sasa Serikali haitakuwa na ‘Msalie Mtume’ kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo.

Alisema, wakati Serikali ikisubiri ujio wa mfumo mpya unaotarajiwa kufungwa katika kipindi cha wiki 16 kuanzia sasa, sambamba na tiketi zilizopo sasa za usafiri wa mabasi hayo kuunganishwa na mifumo ya TRA, DART inapaswa kuwa na njia zaidi ili kulinda mapato hayo.

“Mhakikishe hakuna uvujaji wa mapato kwa kuipitia mara kwa mara mifumo yote na kujiridhisha kuwa ipo salama, pia muendelee kuifanyia ukaguzi na mapitio mifumo yote ya TEHAMA ili kuilinda dhidi ya upotevu huo wa mapato hayo,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa mradi huo wenye mabasi yapatayo 210 ambayo hutoa huduma kwa wananchi kati ya 190,000 hadi 210,000 kwa siku

Vilevile, Waziri Kairuki ameuagiza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka kuhakikisha iwanawaondolea usumbufu wananchi wa kukaa muda mrefu kwevye vituo wakidubiri huduma

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here