Na Mwandishi Maalum
WAANDISHI wa habari ambao bado hawajakidhi vigezo vya kitaaluma vya kupata ithibati wamehimizwa kurejea vyuoni ili kuongeza ujuzi na kufikia viwango vinavyotakiwa katika mfumo wa sasa wa usimamizi wa taaluma hiyo.
Wito huo umetolewa na wadau wa sekta ya habari wakati wa mdahalo wa JAB Day uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba, ndani ya eneo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DAR-PC), Bakari Kimwanga, amesema waandishi wanapaswa kuona elimu kama nyenzo ya kuongeza uwezo wao kitaaluma na si kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akichangia hoja wakati wa mjadala huo, Kimwanga amesema mafunzo ya ngazi ya astashahada na kuendelea yanaweza kuwasaidia waandishi kuongeza ujuzi, kuimarisha weledi na kufikia sifa zinazohitajika katika mfumo wa ithibati.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Elius Msuya ambaye amesema waandishi wanaweza kuendelea na masomo wakiwa kazini ili kuboresha uwezo wao kitaaluma.
Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesisitiza Bodi hiyo imeanza kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa kuhakikisha wanaofanya kazi katika tasnia ya habari wanatimiza masharti ya kitaaluma na kisheria.
Amesema ukaguzi huo umefanyika katika baadhi ya mikoa ikiwemo Dodoma, Iringa na Morogoro kwa lengo la kujiridhisha kuwa waandishi waliopo wana sifa zinazotakiwa.
“Sasa hivi tumeanza kufanya ukaguzi mkoa kwa mkoa kuhakikisha wale waliopo na wanaofanya kazi wamekidhi vigezo vya kitaaluma na kisheria,” amesema.
Kipangula amesema utoaji wa ithibati unategemea uhakiki wa sifa na vigezo vya mwombaji, na kwamba JAB imeendelea kushughulikia masuala yanayohusu utekelezaji wa mfumo huo.
Amesema hadi sasa Bodi hiyo imeshughulikia jumla ya mashauri 19 yanayohusiana na masuala mbalimbali ya ithibati.
Amesisitiza kuwa mtu ambaye hana sifa zinazotakiwa hawezi kurejea katika shughuli za uandishi wa habari au utangazaji hadi atakapokidhi masharti yaliyowekwa.
Mfumo wa ithibati unaendelea kujenga mazingira yanayolenga kuhakikisha sekta ya habari inakuwa na wataalamu wenye sifa, huku waandishi wakihimizwa kuendelea kujifunza na kutumia teknolojia kuboresha taaluma hiyo.
Picha: Imani Nathaniel