CUF watoa msimamo wao kuhusu ripoti ya Kikosi Kazi

0

Na Jumbe Abdallah

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kinaheshimu haki na uhuru wa kila mdau, lakini kimewataka viongozi na wanachama wake kutojiegemeza kwenye misimamo ya vyama vingine vilivyojitokeza kwa misimamo mbalimbali baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Kikosi Kazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Ripoti hiyo yenye mapendekezo 18 iliwasilishwa Oktoba 21, 2022 baada ya kikosi kazi hicho kukusanya na kuchakata Maoni kutoka kwa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini na makundi mbalimbali ya Kijamii na wadau wengine.

Mara baada ya kukabidhiwa kwa ripoti hiyo, wadau mbalimbali wametoa maoni na misimamo yao kupitia mikutano na waandishi wa habari na kwa njia nyingine ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma Eng. Mohamed Ngulangwa, kupitia taarifa yake aliyoitoa Oktoba 23, 2022 alisema CUF kilishiriki kupeleka maoni yake kwenye Kikosi Kazi hicho, hivyo ni vyema wanachama na viongozi wakabaki kwenye hoja ambazo chama hicho kiliwasilisha kwenye Kikosi Kazi.

“CUF ni miongoni mwa vyama vilivyowasilisha mapendekezo yake kwa Kikosi Kazi na tuliweka hadharani mapendekezo yetu kupitia vyombo vya habari na pia kupitia mitandao ya Kijamii. Tunaheshimu haki na uhuru wa kila mdau katika kudhihirisha msimamo wake, uwe wa kuunga mkono au kupinga chochote…”

“Ila wanachama na viongozi wetu watumie hoja za Chama katika maoni yake kwa Kikosi Kazi wakati huu tunapofanya Tathmini na Tafakuri kuhusiana na mapendekezo hayo. Hili ni muhimu sana kwa kuwa litatubakisha katika kukumbatia yetu badala ya kugeuka ‘madalali’ wa misimamo ya wengine,” alisema Ngulangwa.

Aliendelea kusema, “Vyovyote iwavyo, mapendekezo ya Kikosi Kazi hayawezi kufanana nukta kwa nukta na mapendekezo ambayo sisi kama Chama tuliyawasilisha na kuyafafanua. Vipo vyama ambavyo navyo viliwasilisha mapendekezo yao kama tulivyofanya na vipo vyama vilivyogoma kufanya hivyo kabisa.”

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema, chama hicho kinaendelea kuipitia ripoti ya Kikosi Kazi kabla ya kutoa tamko rasmi kuhusiana na ripoti hiyo na wananchi watajulishwa siku ya kuwasilishwa kwa tamko hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here