‘Chadema, ACT Wazalendo vitaendelea kupoteza wanachama kwa kukosa sera’

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

VYAMA vya Chadema na ACT Wazalendo vitaendelea kupoteza wanachama kutokana na kukosa sera za kuwaeleza wanachama wao.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake leo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, wanachama makini wanahama kwasababu hawasikii sera zinazoeleweka kutoka kwa viongozi wa vyama vyao.

“Leo ACT Wazalendo wamezunguka Zanzibar zaidi ya mara saba, lakini wanachosema ni ‘bandika, bandua’, mara Muungano, ooh Mwinyi hapa sio kwao na hadithi za kale za Marehemu Maalim Seif Sharrif Hamad.

“Chadema wao wapo na ‘No reform No Election’ lakini sio watawafanyia nini Watanzania hawasemi, watu wanataka maendeleo yanayoonekana kama ilivyo sasa, sio porojo” alisema.

Alibainisha kuwa, ACT Wazalendo wanasema barabara, maghorofa, nyumba bora za makazi zinazojengwa kwa ajili ya wananchi, viwanja vya michezo, miundombinu ya maji sio maendeleo, lakini hawasemi kitu gani ndio maendeleo.

“Wanataja miji kama Singapore, Dubai hivi huko wanapotaja utatoka Airport njiani ukutane na vibanda vya udongo na makuti?” alihoji Mbeto na kuongeza, mji ukijengeka vizuri unavutia watu kuitembelea, hivyo Serikali inaingiza mapato sio kama wanavyosema wao.

Alisema, ujenzi wa viwanja vya michezo umefanya mchezo wa fainali za CAF kufanyika Zanzibar. “Michuano ya AFCON inakuja Zanzibar hayo sio maendeleo? Wanataka maendeleo gani?”

Alisema, kama alivyofanya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Abeid Amaan Karume, nyumba nzuri za kisasa za makazi wanajengewa wananchi Unguja na Pemba.

“Nyumba zaidi ya 1000 za makazi zinajengwa Chumbuni, 500 Kisakasaka, 3000 Fumba, Furaha na kwingineko,” alisema na kuongeza kuwa, hawana hoja na wangekuwa nayo wangewaeleza wanachama wao.

Alisema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa inatekeleza diplomasia ya Biashara, Uchumi na Uwekezaji na ndio maana imeanzisha miji ya viwanda.

“Rais Mwinyi na Mama Rais wamefanya mambo makubwa sana ya maendeleo” alisema na kutaja miji ya viwanda ya Tanga na Dunga. “Kifupi hivyo vyama vimekosa sera na ndio maaana wanachama makini wanaondoka.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here