CCM yalaani kauli za kuchochea uvunjifu wa amani

0
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM Zanzibar) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, iliyofanyika Mkoa wa Kusini Pemba.

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM amelaani kauli za baadhi ya wafuasi, wanachama na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzi Zanzibar zenye kuhubiri mgawanyiko na kuchochea uvunjifu wa amani.

Shaka alisema hayo wakati wa mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi yaliyofanyika kisiwani Pemba.

“Chama Cha Mapinduzi kinalaani vikali vitendo vilivyoanza kujitokeza siku za karibuni hasa kisiwani Pemba kwa baadhi ya wafuasi, wanachama na viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa kuhubiri mgawanyiko kuchochea uvunjifu wa amani, sio utamaduni wetu wazanzibari, sio utamaduni wetu Watanzania, CCM inalaani vikali, alisema.

Alisema, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Ibara ya 9(a) imeahidi katika kipindi cha miaka mitano kazi kubwa itakayofanywa na CCM ni kuimarisha maridhiano, kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Shaka alisema, kazi hiyo inafanywa vizuri na Rais Dkt. Samia na Rais Dkt. Mwinyi. “Kuweni na amani wana CCM. Hamtajutia kumwani Dkt. Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, nia yake ni kutuvusha.”

Katibu Mwenezi Shaka alisema, Rais Dkt. Samia na Rais Dkt. Mwinyi ni nyenzo muhimu katika kuendeleza mapatano, maridhiano na masikilizano ya kisiasa nchini. “Wameanza vizuri sana kwa sababu wana baraka za Chama Cha Mapinduzi,”

MAMLAKA YA RAIS YAHESHIMIWE

Shaka alisema, uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar haujamwondolea Rais Dkt. Mwinyi Mamlaka ya Kikatiba kufanya shughuli za Kiutawala.

Alisema, Dkt. Mwinyi hapangiwi, bali anashauriwa na kwenye kushauriwa kuna kukubali au kukataa, hivyo ijapokuwa kuna serikali ya umoja wa Kitaifa, lakini Katiba ya nchi lazima iheshiniwe.

“Uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa sio sababu ya kujihalalishia kwamba eti kuna chama kingine ni lazima kishinde uchaguzi hapana. Wenye ulazima wa kushinda uchaguzi ni CCM ambao tumebeba dhamana ya kuwatumikia Wazanzibari tumebeba dhamana ya kuwatumikia Watanzania kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kazi hiyo imefanywa vizuri sana na Dk. Mwinyi,” amesema.

Aidha, alimhakikishia Dk. Mwinyi kuwa Wazanzibari Watanzania kwa ujumla hususan wapenda maendeleo wanamwlewa, hivyo aendelee kuchapa kazi.

“Uwepo wa Serikali ya umoja wa kitaifa sio Jukwaa la fursa na kutaka kuleta mgawanyiko, mfarakano na kuvuruga amani ya nchi hatujafikia huko,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here