Bilioni 80 zatumika kusambaza umeme vijijini mkoani Singida

0

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema zaidi ya Shilingi Bilioni 80 zimetumika kutekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini Mkoani Singida na hivyo kuboresha huduma za kijamii na uchumi kwa wananchi vijijini.

Kapinga alisema hayo mara baada ya kuwasha umeme katika  Kijiji cha Maswauya na Mdilu,  Wilaya ya Singida Kaskazini mkoani Singida.

Akizungumza na Wananchi wa vijiji hivyo, Kapinga alisema lengo la Serikali  ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha inapeleka umeme kwenye Vijiji na Vitongoji vyote ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga fedha ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 4000.

“Serikali inafahamu kuwa kuna vitongoji ambavyo havina umeme lakini maendeleo ni hatua, ilikuwa lazima umeme ufike katika vijiji vyote Tanzania na kisha usambae vitongojini, niwahakikishie kuwa Serikali itapeleka umeme  kwenye maeneo yote.” alisisitiza Kapinga. 

Ameeleza kuwa, kazi nzuri inayofanyika ya usambazaji umeme mijini na vijijini ni  matunda ya uchapakazi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na maono yake ambayo yamewezesha umeme kusambaa kwenye maeneo hayo ikiwemo vijiji 80 vilivyosambaziwa umeme Singida Kaskazini huku vijiji Vinne tu vikisalia ambavyo ifikapo Juni 15, 2024 vitakuwa vimewashiwa umeme.

Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Abedi Ighondo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Abedi Ighondo alisema, Rais Dkt. Samia ametekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kufikisha huduma ya umeme katika vijiji , miradi ya maji, miradi ya afya na elimu na kwamba wamepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi  wa vyumba vya madarasa na Madawati.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Kaskazini, Godwin Gondwe ameahidi kufuatilia utekekezaji wa miradi hiyo ya umeme vijijini ikiwemo kuhakikisha kuwa umeme unafika kwenye maeneo yanayotoa huduma kwa jamii ikiwemo zahanati.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Kaskazini, Godwin Gondwe

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here