MTENDAJI Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, ameahidi kuwa Baraza la Wafanyakazi la UCSAF litaendelea kufanya kazi zake kwa uhuru, kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na masharti ya Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi uliosainiwa na Chama cha Wafanyakazi cha TUGHE.
Mhandisi Mwasalyanda aliyasema hayo leo tarehe 18 Oktoba 2025, wakati wa uzinduzi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa UCSAF, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kwamba Baraza ni chombo muhimu cha kuwakutanisha wafanyakazi na kuwashirikisha kikamilifu katika mipango na maendeleo ya UCSAF, huku wajumbe wake wakitarajiwa kutoa mchango unaolenga kuboresha utendaji wa taasisi.
Aidha, Mhandisi Mwasalyanda amesema UCSAF itaendelea kukusanya maoni, ushauri, na mapendekezo kutoka kwa wafanyakazi wote ili kuboresha utendaji wa Mfuko na kufanikisha malengo yake kwa ufanisi zaidi.