BARAZA la Madiwani wa Halmashauri Wilaya ya Kibaha limepitisha makadirio ya bajeti ya Shilingi Bilioni 39.6 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Makadirio hayo ya bajeti yamepitishwa katika kikao maalumu cha Baraza hilo, kilichofanyika Mlandizi Wilaya ya Kibaha.
Akiwasilisha hoja katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema, kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 30 ni kutoka Serikali kuu, Shilingi Bilioni 4.6 zitatokana na mapato ya ndani na Shilingi Bilioni 4 ni michango ya wafadhili.
Makala alisema, ipo miradi mbalimbali itakayotekelezwa kupitia fedha za ndani ambayo ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya kuhifadhiwa maiti katika kituo cha afya Magindu ambayo imetengewa Shilingi Milioni 50.
Miradi mingine ni ujenzi wa jengo la X- ray katika kituo cha afya Mlandizi uliotengewa Shilingi Bilioni 100 na madawati 200 ambayo yataenda katika shule za Samia Mtongani (100) Boko Mnemela (50) na kawawa (50).
Alisema, katika bajeti ya 2023/2024 Halmashauri ilipokea Shilingi Bilioni 32.8 sawa na asilimia 97 ya makisio ya mwaka ambayo ni Shilingi Bilioni 33.9.
Makala alieleza kwamba, hadi kufikia June 2024 Halmashauri hiyo imepata Mafanikio katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari sambamba na kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa.
Katika Baraza hilo Madiwani wameomba Halmashauri kuangalia namna ya kukarabati barabara kwenye Mitaa yao pamoja na kuongeza idadi ya vyumba vya Madarasa kuwanusuru wanafunzi wasisongamane katika chumba kimoja.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shukuru Lusanjala alisema, bajeti hiyo ikipitishwa watasimamia utekelezaji wake kama ilivyopangwa kwa kuwagusa wananchi moja kwa moja.
Lusanjala pia alisema, kwenye maeneo yaliyoelezwa kuwa na barabara mbovu, uhitaji wa madawati na vyumba vya Madarasa watatafita namna ya kutatua kupunguza upungufu uliopo.