NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdi Mahamoud Abdi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kuondosha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ndugu Abdi ameyasema hayo leo, Septemba 23, 2026, katika kuendeleza ziara yake ya kukagua uhai wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo la Mahonda, ambapo amepata fursa ya kufungua kisima cha maji safi na salama kilichojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Mbunge wa Jimbo la Mahonda.
Amesema, kisima hicho kitasaidia kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama wananchi wa Boma, Shehia ya Pangeni.
Aidha, Abdi amempongeza Mbunge wa Jimbo la Mahonda kwa dhamira yake ya dhati ya kushirikiana na wananchi katika kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Katika hatua nyingine, Abdi amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo ya maji ili iweze kuendelea kuwa na tija na kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya wananchi.
Wakati huohuo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa kunyesha, hususan mvua za El nino, na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa pamoja na kuchukua hatua stahiki za kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo Othman Maulid Suleiman amesema, afisi yake kwa kushirikiana na mwakilishi wanampango wa kuchimba visima 12 vitakavyotatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbali mbali ya jimbo la Mahonda.