▪️Awataka wachimbaji wote nchini kuzingatia sheria na kanuni za madini
▪️Alekeza Maafisa Madini kusimamia sheria ili kupunguza migogoro kwenye sekta ya Madini
📍Dodoma
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amewataka wachimbaji kote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Mavunde ameyasema hayo jana Jijiji Dodoma wakati wa kikao cha kutatua mgogoro wa mipaka ya Leseni uliyopo kati ya Kampuni ya Njake na Patrick Miroshi, ambapo alizikutanisha pande zote mbili zenye mgogoro huo na kujadili kwa pamoja namna ya kutatua mgogoro huo na mwishoni kufikia muafaka wa kila mmoja kuendelea na uchimbaji katika eneo la leseni yake kwa amani.
“Serikali inatamani kuona Sekta ya Madini inaendelea kukua na kutoa mchango wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, migogoro siku zote inaturudisha nyuma katika jitihada za kuongeza uzalishaji na kuchochea Uchumi.
Ni maelekezo ya Mh. Rais Dkt. Samia
S. Hassan juu ya utatuzi wa haraka wa migogoro kwenye sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wake.
Niwatake maafisa Madini wote nchini kusimamia sheria na kanuni ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima na pia niwatake wachimbaji wote kuzingatia sheria katika shughuli zao za kila siku”, alisema Mavunde.
Baada ya Taarifa ya Timu ya wataalamu iliyoundwa na Waziri Mavunde ilielekezwa nankuridhiwa kuwa Pande mbili hizo kila mmoja kurejea kwenye eneo la mipaka ya Leseni yake na Kampuni ya Njake kumfidia Miroshi gharama alizoingia awali za uchimbaji.
Kikao hicho cha usuluhishi kilihudhuriwa na viongozi wa Wizara akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo.