‘Miaka 61 ya Mapinduzi Pemba imetia fora’

0

Na Mwandishi Maalum, Pemba

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewashukuru wananchi wa Kisiwa cha Pemba kwa kujitokeza kwa wingi mwanzo hadi mwisho kwa kushiriki kwao katika uzinduzi wa miradi ya maendeleo na kuhudhuria kwa wingi mikutano ya hadhara ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Pia, kimesema kushiriki kwao huko ni kielelezo wananchi wote wa Pemba wana imani kutokana na uchapakazi wa Serikali ya Awamu ya Nane kwa kuimarisha huduma jamii.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenzi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema ushiriki wa wananchi wa Pemba mwaka huu umetia fora na kuvunja rekodi.

Mbeto alisema, wananchi hao bila kujali itikadi za kisiasa, walijitokeza kwa wingi kila walipoitikia wito wa chama na Serikali wa kuhudhuria shughuli muhimu za uzinduzi wa miradi ya kimaendeleo.

Alisema, wananchi wa Mikoa miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba, wakazi wote katika Wadi, Majimbo na Wilaya za mikoa miwili ya Pemba, hawakuona muhali badala yake wamekuwa mstari wa mbele kuonyesha upendo, hisia na furaha zao.

“Ni sherehe za aina yake za miaka 61 ya Mapinduzi. Pemba imetia fora. Wananchi wamehudhuria shughuli zote ikiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Pia, wamejitokeza kwa wingi katika kilele cha maadhimisho Uwanja wa Gombani,” alisema Mbeto.

Aidha, alisema ni wazi kuwa wananchi wameridhishwa na utendaji wa SMZ Awamu ya nane, unaojali maslahi ya umma, utekelezaji wa mirdi na ahadi za Serikali ulioondosha kero zilizokuwa zikiwakabili wananchi.

“Imani siku zote huzaa imani. Nyota njema huanza kuonekana mapama asubuhi. Wananchi wa Pemba kwa kumuunga kwao mkono Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwalipa utumishi uliotukuka” alisema Mwenezi huyo.

Mbeto aliwataka wananchi wa Zanzibar kuanza kutafakari na kupuuza siasa zisizoitakia mema nchi yao kutokana na tamaa binafsi za baadhi ya wanasiasa ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma nchi yao kimaendeleo.

“SMZ chini ya sera za CCM itaendelea na mikakati ya kuwatumikia wananchi wote bila upendeleo wa aina yoyote. Kazi ya kupeleka huduma muhumu za kijamii itasimamiwa na uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi,” alieleza.

Hata hivyo, Mbeto aliwataka wananchi wa Pemba kuendelea kuiunga mkono Serikali yao ya Awamu ya nane na ifikapo Oktoba, mwaka huu wajiandae kumchagua Rais, madiwani, wawakilishi na wabunge toka CCM.

“Wananchi wa Pemba kinadharia na kiuhalisia wameamka na kutuma ujumbe mzito kwa upinzani .Muda na nyakati zimebadilika. Pepo zinazovuma pemba ni mpya za wito wa matumaini mapya kwa maendeleo,” alieleza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here