Wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa Taifa linawategemea – Katimba

0

Na Angela Msimbira, GEITA

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Zainab Katimba ametoa rai kwa wanafunzi wote nchini kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufaulu kwa viwango vya juu ili badae walitumikie taifa.

Katimba ametoa rai hiyo alipotembelea shule mpya maalum ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita kwa lengo la kukagua miundombinu iliyojengwa na kujionea maboresho yaliyofanywa na Serikali katika ujifunzaji na ufundishaji kwenye sekta ya elimu nchini.

Alisema, dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu iliyobora katika mazingira mazuri hivyo ni wajibu wa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.

“Namna pekee ya kumlipa Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha na kujenga miundombinu iliyobora na kuhakikisha mnapata elimu bila ada ni kuhakikisha na ninyi mnasoma kwa bidii, mfaulu vizuri na kupata elimu bora ili baadaye muweze kulitumikia taifa.”

Katimba alisema, wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa Taifa linawategemea, hivyo amewataka kuhakikisha hawafanyi mchezo wakiwa shuleni bali watumie fursa hiyo kujenga kesho yao.

Akitoa taarifa ya elimu Mkoa wa Geita, Katibu Tawala Mkoa huo, Mohamed Gombati alisema kwa upande wa shule ya sekondari ya wasichana imepokea Shilingi Bilioni 3 katika awamu ya kwanza na Juni mwaka huu zimepokelewa Shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo na tayari imeshaanza kuchukua wanafunzi.

Alisema, kwa mwaka 2021/22 Mkoa wa Geita ilipokea Shilingi Bilioni 17, mwaka 2022/23 zilipokelewa Shilingi Bilioni 31 na kwa mwaka 2023/24 zilipokelewa Shilingi Bilioni 32 bila kujumuisha fedha zinazotolewa kugharamia elimu bila ada.

Alisema, katika fedha za ndani zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo za asilimia 60 au 40 kiwango kikubwa kinaelekezwa kwenye sekta ya elimu.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita, Mwamin Kagoma alisema shule hiyo imegharimu Shilingi Bilioni 4.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here