UCHUMI wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na pia huko Mashariki ya Kati. Matatizo haya yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya 7% na kuushusha hadi 4.2% mwaka 2020.
Hata hivyo, hivi sasa ukuaji umefikia 5.2% kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa Pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka (GNI per capita) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200.
Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya 4% – kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Vile vile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4. Akiba hiyo ni sawa na Dola za Marekani Bilioni 5.4.
UKUSANYAJI MAPATO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu hii kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara na kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi. Hivyo basi, makusanyo yamefikia Shilingi 2 Trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23 kutoka Shilingi Trilioni 18.15 mwaka 2020/21. Hili ni ongezeko la Shilingi Trilioni 5.99.
Aidha, kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni Shilingi Trilioni 2.13. Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia tarehe 20 Machi, 2024, TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 19.21, ikiwa ni dalili kwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita.
UWEKEZAJI
Katika kipindi mwaka Machi 2021 hadi Machi 2024 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani Milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464. Kati ya miradi hiyo asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya Wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na Wageni.
Aidha, Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uwekezaji (National Investment Steering Committee – NISC) ilitoa idhini ya kusainiwa mikataba ya utekelezaji kwa miradi 16. Miradi hiyo yenye hadhi ya mirahi mahiri ni pamoja na Mradi wa Bagamoyo Sugar Limited; Mradi wa Kagera Sugar Limited; na Mradi wa Mtibwa Sugar Estate Limited;
Vile vile, NISC iliridhia miradi mingine nane ambayo ilisaini mikataba ya utekelezaji na TIC, yaani (perfomance contracts) baada ya kupewa hadhi ya kuwa wawekezaji mahiri maalum.
Katika kundi hili kuna wa upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari wa Kampuni ya Kilombero Sugar Limited; na pia Mradi wa kilimo cha miwa na kiwanda cha kuzalisha sukari wa Kampuni ya Mufindi Paper Mills Limited – Kasulu.
OFISI YA MSAJILI WA HAZINA
Thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi Trilioni 76 mwaka 2023 – sawa na ongezeko la 8.6%.
Sababu ya ongezeko hili ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha Shilingi Trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.
Aidha, Ofisi pia imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka Shilingi Bilioni 637.66 hadi Trilioni 1.008 kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la 58%.
Serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka 25% hadi 37% huku ikisaini mikataba ya ubia wa 16% zisizohamishika katika kampuni za madini.
SEKTA YA MADINI
Katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Februari 2024 Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.93. Awali mwaka 2021/22 ilikuwa Shilingi Bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia Shilingi Bilioni 690.4.
Aidha, katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa Shilingi Bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia Shilingi Bilioni 476.8.
KILIMO
Bajeti imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 294.16 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni Shilingi Bilioni 970.78 mwaka wa fedha 2023/2024. Matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 320,233 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani 580,628 kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi Shilingi Bilioni 361.5 mwaka 2023/24 ambapo wataalam wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika ofisi za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 139. Mitambo 15 na magari 53 vimenunuliwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji.
Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023. Aidha, Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa skimu zaumwagiliaji zenye hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 pamoja na kuanza skimu mpya zenye ukubwa hekta 95,000 kwa mwaka 2023/2024, ambapo kukamilika kwake kutaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 917,280.
Programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Build Better Tomorrow-BBT). Mradi unashirikisha vijana 688, ambao wameanza kilimo biashara katika shamba la Chinangali II.
UFUGAJI NA UVUVI
Katika kipindi cha miaka mitatu 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya mifugo imekua ikiongezeka kwa kasi. Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Shilingi 47,844,950,000/-mwaka 2021/22 hadi Shilingi 112,046,777,000/- mwaka 2023/24.
Katika kipindi cha miaka mitatu, 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya uvuvi imepanda kutoka Shilingi 121,350,046,999/- mwaka 2021/22 hadi Shilingi 183,874,156,000 mwaka 2023/24.
Ili kuhakikisha Serikali inarasimisha shughuli za uvuvi, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Januari 30, 2024, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua zoezi la ugawaji wa boti 160 na vizimba 222, kwa ajili ya makampuni, watu binafsi na vikundi vya wavuvi kupata vitendea kazi hivyo kwa njia ya mkopo usio na riba. Sasa bandari ya uvuvi inajengwa Kilwa Masoko.
UTALII
Hii ndiyo sekta inayoongoza hivi sasa kwa kuiletea nchi fedha za kigeni ambapo sasa zimefikia dola za Marekani Bilioni 3.37 (zaidi ya shilingi trilioni 8). Kimsingi sekta hii imemrejeshea shukurani Mhe. Rais kwa juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji wa filamu ya “Tanzania: The Royal Tour”.
Katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato Dola za Marekani Bilioni 1.31hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza Dola Bilioni 3.37.
Kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya mlipuko wa UVIKO-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia; na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya Moroko na Morisi (Mauritius).
Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali. Tuzo hizo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2023; Tanzania kuwa nchi ya saba miongoni mwa nchi 18 duniani zilizo bora kutembelewa kiutalii kwa mwaka 2022; Hifadhi ya Taifa Serengeti kuorodheshwa kama eneo maridhawa la kutembelewa kwa mwaka 2023; na Hifadhi ya Taifa Serengeti kushika nafasi ya tatu ya vivutio bora vya asili duniani kwa mwaka 2023.
Aidha, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeshinda tuzo mbili za Best of the Best Travelers’ Choice na Africa’s Leading Tourist Destination kwa mwaka 2023. Hizi ni baadhi ya tuzo ambazo Tanzania imezipata kimataifa; si zote.
MIUNDOMBINU NA UCHUKUZI
Reli ya Kisasa (SGR)
Itakumbukwa kwamba mara alipoingia madarakani, Mhe. Rais aliahidi kumalizia ujenzi wa vipande vilivyoanzishwa na awamu ya tano sambamba na kuanza kwa ujenzi kwa vipande vya Makutupora-Tabora (km 368), Tabora-Isaka (km 165), Isaka-Mwanza (km 341) na TaboraKigoma (km 506).
Wakati huo kipande cha Dar es Salaam-Morogoro kilikuwa kimefikia 83.55% na cha Morogoro – Makatupora 57.57% vikiwa na jumla ya Kilomita 722. Hadi sasa utekelezaji umefikia 98.90% kwa kipande cha kwanza na 96.51% kwa kipande cha pili. Tayari fedha zimeshalipwa kiasi cha Shilingi Trilioni 6.805 kati ya Shilingi Trilioni 7.4 zilizotakiwa.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilianzisha ujenzi wa vipande vitano vipya ambapo vitatu ni katika kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Mwanza, yaani Makutupora hadi Tabora (KM 368) ambapo ujenzi umefikia 13.98%; Tabora hadi Isaka (KM 165) sasa ujenzi umefikia 5.44%; na Isaka hadi Mwanza (KM 341) ambapo ujenzi umefikia 31.07%.
Aidha, ujenzi wa Awamu ya Pili umeanza kwa vipande vya Tabora hadi Kigoma (KM 506) na kwa Uvinza hadi Musongati (km367) hivi sasa taratibu za ununuzi zinaendelea. Hii inafanya jumla ya Kilomita 1,560 za ujenzi wa SGR kutekelezwa ndani ya serikali ya awamu ya sita – sawa na 68.4% ya ujenzi unaoendelea.
Thamani ya uwekezaji huu imefikia Trilioni 23.3 ukiondoa kipande cha Uvinza hadi Musongati ambacho kipo katika hatua ya ununuzi. Jumla ya Shilingi Trilioni 10.1 zimeshalipwa kwa wakandarasi kwa mujibu wa hati za malipo na malipo ya awali kwa vipande vipya.
Serikali pia inafanya ununuzi wa treni za kisasa (EMU) seti 10; mabehewa ya abiria 89; na mabehewa ya mizigo 1,430. Uwekezaji huu una thamani ya dola za Marekani Milioni 508.6 – sawa na Shilingi Trilioni 1.2.
Ikumbukwe kwamba Mhe. Rais alishatoa maelekezo kuhakikisha reli hii mpya inayafikia masoko ya kikanda kwa nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ili kuleta manufaa makubwa. Juhudi zinaendelea na makubaliano na nchi hizi yameshafikiwa ili reli itoke Uvinza, Tanzania, iende hadi Kindu nchini DRC kupitia Musongati-Gitega-Bujumbura nchini Burundi.
BANDARI
Meli ziliongezeka kutoka 4,318 Machi 2021 hadi kufikia meli 4,762 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 10.28. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 11.79 kwa mwaka.
Shehena iliyohudumiwa iliongezeka kutoka tani Milioni 17.287 Machi 2021 hadi kufikia tani Milioni 26.544 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 37.9. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 15.4 kwa mwaka. Shehena za makasha na shehena za magari ziliongezeka.
Shehena ya nchi jirani iliongezeka kutoka tani 6,166,052 Machi 2021 hadi kufikia tani 9,452,535 Februari 2024, sawa na ongezeko la asilimia 53.3. Kiwango hiki cha ukuaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 26.5 kwa mwaka.
Katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali imeweza kukamilisha yafuatayo:-
- Ujenzi wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari (Gati Na. 0);
- Uboreshaji wa gati Na. 1 – 4 kwa ajili ya kuhudumia shehena mchanganyiko,
- gati Na 5 – 7 kwa ajili ya kuhudumia shehena ya makasha,
- kuongeza kina cha gati 1-7 kutoka mita 11 hadi kufikia mita 14.5, na;
- kukamilika kwa ujenzi wa yadi ya kuhudumia makasha;
- kuchimba na kupanua lango la kuingilia meli na sehemu ya kugeuzia meli
Mbali ya Serikali kuongeza vifaa vya kisasa, lakini pia kuna upanuzi wa bandari za Tanga, Mtwara, na zile za maziwa ili kukidhi mahitaji ya soko katika nchi jirani ambayo yanaongezeka siku hadi.
USAFIRI WA ANGA
Serikali iliendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwekeza zaidi ikiwemo kununua ndege ili kulifanya limudu kutoa huduma na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi.
Katika miaka mitatu Serikali imenunua ndege tano zikiwemo tatu za masafa ya kati ambazo ni Airbus A220 mbili; Boeing 737 Max9; Boeing 767-300F ya mizigo na Dash 8 Q-400 na zote zinaendelea kutoa huduma.
Ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max9 (iko katika hatua ya makabidhiano) na moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 (katika hatua ya uundwaji) tayari zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
Hivyo basi, kwa kujumuisha na uwekezaji huu sasa ATCL ina jumla ya ndege za abiria 12 na moja ya mizigo zinazohuduma vituo 24 kutoka vituo 19 vya mwaka 2021 na inatarajiwa vitaongezeka.
Kwa ujumla wake, ATCL imeongeza abiria kutoka 537,155 mwaka 2021 hadi 1,070,734; tani za mizigo 1,290 mwaka 2021 hadi 3,561; na miruko 10,550 mwaka 2021 hadi 17,198 mwaka 2023.
UJENZI WA BARABARA
Katika Kipindi cha miaka mitatu (2021 -2024), Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanikiwa kukamilisha miradi 25 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,198.50. Katika kipindi hicho, jumla ya barabara 57 zenye urefu wa kilometa 3, 794.1 ziko hatua mbalimbali za utekelezaji.
Kadhalika, miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa nane imekamilika. Aidha, miradi mitano ya ujenzi wa madaraja inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kielelezo wa ujenzi wa daraja la J. P. Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza lenye urefu wa Mita 3,200 kwenye ziwa Victoria likiunganisha mji wa Mwanza na mikoa ya Geita na Kagera.
Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza miradi ya viwanja vya ndege ambapo vitano vimekamilika, miradi nane inaendelea chini ya TANROADS. Miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege inayoendelea ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ambacho kinajengwa kwa fedha za Serikali (GOT) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
BARABARA MIJINI NA VIJIJINI
Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya uboreshaji miundombinu chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na kufikia jumla ya Shilingi Trilioni 2.53 katika kipindi cha miaka mitatu. Fedha hizi zimewezesha ujenzi wa barabara za lami za Kilomita 819.22 (tofauti na barabara za lami zilizo chini ya TANROADS) na hivyo kuongeza mtandao wake kutoka Kilomita 2,404.90 hadi 3,224.12.
Kwa upande wa barabara za changarawe, jumla ya Kilomita 11,924.36 zimejengwa na kuongeza mtandao wake kutoka Kilomita 29,183.36 hadi 41,107.52. Kumekuwa pia na ujenzi wa madaraja mengi nchini ikiwemo kutumia teknolojia ya mawe.
Aidha, TARURA imepokea wito wa Mhe. Rais wa kuhakikisha sasa inatumia teknolojia mbadala ambapo majaribio ya teknolojia ya ECOROADS yameonesha mafanikio makubwa ambapo Kilomita 22 zilijengwa katika eneo korofi na teknolojia hii kuhimili changamoto za eneo hilo.
UZALISHAJI UMEME
Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kihistoria wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP). Mradi huu utakuwa na vinu tisa vyenye uwezo wa kuzalisha Megawati 235 kila kimoja na kufanya jumla ya Megawati 2,115. Ikumbukwe kwamba uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme katika nchi yetu hivi sasa ni Megawati 1,911 tu.
Wakati Mhe. Rais Dkt. Samia anaingia madarakani, ujenzi wa bwawa hili ulikuwa umefikia 33% lakini hivi sasa umekamilika kwa 96.28%. Kinu Na. 9 kimeshawashwa na Na. 8 kinatarajiwa kuwashwa mwezi huu kikifuatiwa karibuni na kinu Na. 7. Mradi huu mkubwa wa umeme wa Julius
Nyerere (JNHPP) unagharimu Shilingi Trilioni 6.5 na mpaka sasa serikali imeshamlipa mkandarasi Shilingi Trilioni 5.7 – sawa na 88.7%. Miradi mingine ni ya ujenzi wa njia kubwa za kusafirisha umeme ambazo zitaunganisha mikoa mbalimbali hadi nchi jirani ambapo kutaiwezesha Tanzania kuuza nishati hiyo nje ya nchi pindi itapozalisha umeme wa ziada.
Nchi hizo ni Uganda; Kenya itakayounganisha hadi Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan na Misri pamoja na Zambia itakayounganisha umeme wa Tanzania na wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Aidha, chini ya TANESCO miradi ya vyanzo vingine inafanyiwa kazi ili hatimaye Tanzania ifikie uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo mwaka 2035.
UMEME VIJIJINI
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeunganisha jumla ya vijiji 5,481 na kufikisha vijiji vyenye kuwa 11,843 – sawa na 96.14% ya vijiji vyote nchini ambavyo ni 12,318.
Vile vile, vitongoji 5,562 vimefikishiwa huduma ya umeme na kufanya jumla kuwa vitongoji 32,750 (51%) ya vitongoji vyote nchini ambavyo ni 64,760. Inatarajiwa kwamba kabla ya mwaka 2025 kumalizika, vitongoji vingine 8,150 vitakuwa vimefikishiwa umeme.
MAJI
Lengo la Serikali ni kufikia kiasi cha upatikanaji maji cha 85% kwa vijijini na 95% kwa mijini kufikia mwaka 2025. Katika kufikia malengo haya, ndani ya miaka mitatu iliyopita jumla ya miradi 1,633 ya usambazaji maji imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi waishio katika vijiji 2,534. Hivi sasa jumla ya vijiji 9,259 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini vinapata maji, sawa na 75.2%.
Kwa upande wa mijini kuna jumla ya miradi 213 ya usambazaji maji na usafi wa mazingira ambayo imefikisha huduma kwa wakazi 6,236,015 kwa kutumia gharama ya shilingi bilioni 483.7 na miradi mingine zaidi bado inakuja.
HUDUMA ZA KIJAMII
Huduma za Afya
Uwekezaji katika sekta ya afya kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifikia jumla ya Shilingi Bilioni 916.6 katika miaka mitatu ambapo zililenga kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya msingi. Matunda ya fedha hizi ni:
i. Ujenzi na uendelezaji wa hospitali mpya za halmashauri 127 ambapo kati ya hizo hospitali 25 zimeanza kujengwa kipindi cha awamu ya sita;
ii. Ukarabati wa hospitali kongwe 50 za halmashauri;
iii. Ujenzi wa vituo vya afya 367;
iv. Ukamilishaji wa majengo ya zahanati 980;
v. Ujenzi wa majengo 83 ya kutolea huduma za dharura (EMD), majengo 28 ya huduma
kwa wagonjwa mahututi (ICU) na ujenzi wa kituo cha kutibu magonjwa ya milipuko;
vi. Ujenzi wa mitambo 21 ya kuzalisha oksijeni kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wa dhararua;
vii. Ujenzi wa nyumba za watumishi 270;
viii. Ununuzi wa vifaa vya tiba zikiwemo mashine za mionzi ya X za kidigitali;
ix. Kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya 17,137;
x. Ununuzi wa magari 528 yakiwemo ya kubebea wagonjwa 316.
Kwa ujumla wake, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya, Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa 327 yameshapokelewa na kusambazwa
nchini.
Lakini pia Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza fedha za ruzuku ya kununulia dawa kutoka Bohari Kuu (MSD) ambapo kwa mwaka 2021/22 ilikuwa Shilingi Bilioni 29.3 lakini kufikia mwaka 2022/23 zimefikia Shilingi Bilioni 120.8. Kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 tayari Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 74.5 na Serikali inaendelea kutoa zaidi.
Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024 – ongezeko la vituo 1,061 (12.4%).
Mgawanyo hadi kufikia Machi 2024 ni kama ifuatvyo: Zahanati 7,999; Vituo vya afya 1,170; Hospitali za halmashauri 172; Hospitali zenye hadhi ya wilaya 181; Hospitali za rufaa za mikoa 28; Hospitali zenye hadhi ya mkoa 36; Hospitali za rufaa za kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya kanda 12; Hospitali maalum 6 na Hospitali ya taifa moja.
Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, nchi yetu imevutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi. Kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa wagonjwa 75 mwaka 2021.
Wagonjwa hawa wanatoka katika nchi za Komoro, Malawi, Burundi, Zambia, DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya. Wagonjwa hawa walihudumiwa katika hospitali sita ambazo ni: Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI) na hospitali binafsi za Aga Khan na Saifee.
ELIMU
Bajeti ya sekta imepanda kutoka Shilingi Trilioni 4.72 mwaka 2020/21 hadi Trilioni 5.98 mwaka 2023/24. Aidha, bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya imepanda kutoka Shilingi Bilioni 464 hadi Bilioni 786 mwaka 2023/24. Sasa wanufaika ni 220,278 kutoka 142,170.
Serikali pia imeongeza fursa mbalimbali za elimu ya juu ikiwemo sayansi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi na Serikali imepata mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola Milioni 425 Shilingi bilioni 972). Vyuo vikuu pia vinajenga kampasi katika mikoa ya pembezoni ili kufikisha elimu ya juu nchi nzima.
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika kuimarisha utoaji wa elimu ya msingi na sekondari ambapo kwa kipindi cha miaka miwili jumla ya Shilingi Trilioni 1.29 zilitolewa kupitia miradi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu.
Katika kuimarisha elimu ya awali na msingi, Serikali imejenga shule za msingi mpya 302 hii ikiwa ni mbali na miradi mingine iliyoongeza madarasa na hata mabweni.
Katika kuimarisha elimu ya sekondari, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa jumla ya sShilingi Bilioni 837.8 kupitia vyanzo mbalimbali kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za sekondari. Jumla ya walimu 37,473 waliajiriwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu.
UHAMAJI WA HIARI KUTOKA NGORONGORO
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ndipo Serikali ilichukua uamuzi wa kuliokoa eneo la hifadhi ya Ngorongoro baada ya Kilomita za mraba 3,700 katika 8,292 kuathirika na shughuli za kibinadamu kwa sababu tangu ilipoanzishwa, binadamu na mifugo walikuwa sehemu ya viumbe wanaoishi hifadhini humo.
Hatua hii inajumuisha uhamaji wa hiari kutoka eneo hilo kwenda popote nchini lakini hususani katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga. Serikali imetenga maeneo zaidi katika wilaya za Kilindi na Simanjiro yanayoungana na Msomera.
Hadi kufikia tarehe 19 Machi, 2024, jumla ya kaya 1,195 zenye watu 7,378 na mifugo 33,062 zilikuwa zimehama kwa hiari ambapo katika hizi, kaya 1,079 zilihamia Msomera na 116 zilichagua kwenda kwenye maeneo mengine ndani ya nchi.
Naomba kusisitiza, hili ni zoezi la hiari na si vinginevyo na wananchi wanafanya maamuzi kwa kuzingatia ugumu wa maisha yao ndani ya Ngorongoro na ubora wa maisha mapya huko Msomera. Serikali inatoa fidia ya mali za familia na usafiri hadi Msomera; nyumba kwenye ekari 2.5; shamba la ekari 5; na pia malisho, majosho, maji, mnada, shule, vituo vya afya, barabara, umeme na mawasiliano.
KATIBA NA SHERIA
Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo maalum katika suala la haki ambapo kwanza, imeanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo hadi kufikia Januari 2024, ilikuwa imesaidia wananchi 415,280 katika halmashauri 42 za mikoa sita pamoja na wafungwa na mahabusu 7,166.
Vile vile, jumla ya mashirika 256 yamesajiliwa kwa ajili ya kutoa huduma msaada wa kisheria kwa wananchi bila kuwatoza gharama. Aidha, Serikali imeongeza mawakili kutoka 381 waliokuwepo mwaka 2021 hadi 663 pamoja na waendesha mashitaka kutoka 783 hadi 1,095 –hii yote ili kuhakikisha haki inapatikana.
Kutokana na umahiri wa Serikali katika kujali haki za binadamu na kuheshimu utawala wa sheria nchini, Tanzania imefanikiwa kuwa mwenyeji wa mikutano ya kikanda na kimataifa ya masuala haya ikiwa ni Kikao cha 77 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa nchi za Jumuiya ya Madola.
Lakini pengine mafanikio ya kipekee yaliyopatikana kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni ya kuokoa fedha za nchi katika kesi mbalimbali za madai ndani na nje ya nchi. Kati ya Machi 2021 hadi Februari 2024, Serikali imeokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 860.6.
HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI
Tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani Machi 2021, kumekuwa na uhuru mkubwa wa kujieleza na kutoa maoni kwa njia mbalimbali kama vile kupitia vyombo vya habari na majukwa mabalimbali ya kuhabarisha umma. Kwa amri ya Mhe. Rais, Serikali iliyafungulia na kuyapa leseni mpya za uchapishaji magazeti ya Mwanahalisi, Mawio, Mseto, na Tanzania Daima yaliyokuwa yamefungiwa kwa muda mrefu.
Wakati serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani Machi, 2021 kulikuwa na machapisho 266. Kutokana na uhuru uliopo sasa, jumla ya machapisho 351 yana leseni – ongezeko la machapisho 87 ingawa si yote yanayochapishwa kutokana na kiutendaji au kifedha.
Baada ya Sheria ya Huduma za habari kupitishwa mwaka 2016, wadau walikuwa na maoni tofauti ambayo yaliyotaka mabadilko kadhaa. Wizara kwa kushirikiana na wadau ilifanya mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 na Kanuni zake na hatimaye ikarekebishwa Juni 2023 na baada ya Serikali kupokea maoni ya wadau, Waziri akizisaini Kanuni mnamo Januari 2024.
Serikali pia inaendelea na ukamlishaji wa hatua muhimu za utekelezaji wa sheria hii ikianzia na uundaji wa Bodi ya Ithibati ambayo itawezesha uundaji wa Baraza Huru la Vyombo vya Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari.
Marekebisho haya yamewaondoa wanahabari katika makosa yanayohusiana na kashfa za kijinai, makosa ambayo kwa kawaida yanaangukia katika utaratibu wa mashauri ya madai. Vile vile, adhabu kwa wamiliki wa mitambo ya uchapishaji, ambao katika hali ya kawaida, hawana uwezo wa kudhibiti maudhui yanayochapishwa katika mitambo hiyo ya uchapishaji zimeondolewa.
Wizara inaendelea na kazi ya kuboresha Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003. Maboresho haya yanafanyika kutokana na maoni ya wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji kwamba inahitaji kuendana na wakati.
Vile vile, kufuatia maelekezo ya Mhe. Rais ya Januari 2023, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye aliteua kamati ya kutathmini hali ya utendaji na uchumi kwenye vyombo vya habari na kueleza kuwa dhamira ya Serikali ni kushughulikia suala la uchumi kwa vyombo vya habari. Kamati hiyo imeshakamilisha kazi hiyo na taarifa yake inatarajia kuwasilishwa kwa Mhe. Rais kwa ajili ya maelekezo yake.
Ili kuboresha mawasiliano nchini, Serikali ya Awamu ya Sita iko katika hatua za mwisho za kuandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa. Mkakati huu wa Mawasiliano wa Taifa una lengo la kuhakikisha kuwa wadau katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali ili kukuza utoaji wa huduma za umma kwa maendeleo endelevu. Mkakati huu ni wa miaka mitano na utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo.
Serikali pia imefanya Operesheni ya Anwani za Makazi ambapo hadi sasa jumla ya anwani 12,810,353 zimesajili. Serikali pia kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imefanikiwa kupata fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 126 kwa ajili ya ujenzi wa minara mipya 758 katika kata 713 ili kuwezesha wananchi Milioni 8.5 kupata huduma za mawasiliano; na kupandisha hadhi minara 304 kutoka 2G kwenda teknolojia ya 3G na 4G.
Mkongo wa Taifa pia umeongezewa mtandao wake kwa ujenzi ambapo sasa unafikia wilaya 67 nchini kutoka 36 mwaka 2020/21. Mkongo huu sasa utakuwa na wigo wa Kilomita 3,000 na umeongezwa nguvu zake mara 10 zaidi kutoka Gbps 200 hadi Tbps 2,000.
Serikali pia imeongeza idadi ya wataalam wa TEHAMA kutoka 365 hadi 1,473; na pia kukamilisha utafiti kuhusu Mwongozo wa Tanzania ya Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2023 kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).
Serikali pia inajenga mifumo mikuu mitatu: Mfumo wa utambuzi kidijitali wa jamii namba; Mfumo wa utambuzi wa wateja (e-KYC) na mfumo wa ubadilishanaji taarifa kati ya sekta za umma na binafsi.
Serikali imefanikiwa kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 na hatimaye kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Aidha, mwaka 2021 Tanzania ilishika nafasi ya pili barani Afrika kwa ubora wa usalama mtandaoni kwa mujibu wa ripoti ya GCI (Global Cybersecurity Index) itolewayo na Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (ITU) kila baada ya miaka mitatu.
Kwa dunia nzima Tanzania ilishika nafasi ya 37 kati ya mataifa 182 yaliyofanyiwa tathmini. Chini ya wizara inayosimamia TEHAMA, Serikali imeanzisha Kitengo cha usalama wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuhakikisha taifa linabakia salama.
HIFADHI YA JAMII
Mhe. Rais katika miaka yake mitatu amefanya mengi katika eneo hili lakini moja kubwa ni la kutambua deni la michango ya watumishi wa serikali chini ya uliokuwa PSPF kabla ya Julai 1999. Deni hilo lilitokana na mfuko kulipa wastaafu kuanzia mwaka 2004 kwa muda wote wa ajira zao lakini bila michango yao kuwepo kutokana na mfumo wa zamani ulivyokuwa.
Deni lilifikia Shilingi Trilioni 4.6 na mfuko kuyumba. Desemba 2021 baada ya kuingia madarakani, Mhe. Rais alilitatua tatizo hilo kwa kutoa hati fungani (non-cash bond) ya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.17 na kuokoa hali ya hifadhi ya jamii na hivyo PSSSF kusimama.
UHUSIANO WA KIMATAIFA, ULINZI NA USALAMA
Ushirikiano Kimataifa
Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha hadhi ya Tanzania kimataifa inadumu na kubakia mahali inapostahili. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara chache za kitaifa na kikazi lakini za kimkakati na zenye malengo mahsusi kwa maslahi ya nchi. Mhe. Rais alihudhuria pia mikutano ya kimataifa kama COP 27 nchini Misri na COP 28 kwenye Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na kikanda kwenye jumuiya kama SADC na EAC ili kutetea maslahi ya nchi.
Ziara hizi zimeipatia fursa nyingi nchi yetu pamoja na fedha na kuiweka katika hali nzuri zaidi kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi kufaidika zaidi katika siku zijazo.
Mhe. Rais alianza kazi yake hii kwa kuhakikisha kwanza anaimarisha uhusiano na jirani zetu; hivyo basi, nchi za kwanza kuzitembelea mwaka 2021 zilikuwa katika mtiririko ufuatao: Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Rais pia ameshazitembelea nchi jirani zetu za DRC, Msumbiji, Malawi na Zambia. Hii ina maana nchi zote tunazopakana nazo, tayari Rais wetu ameshahakikisha tunadumisha nazo uhusiano mzuri.
Aidha, ameshafanya ziara katika nchi rafiki kama na Marekani, China, Misri, Oman, Qatar, India na Indonesia pamoja na nchi zingine ambazo tuna uhusiano nazo wa kimkakati ikiwemo kuzitembelea wakati wa kuhudhuria mikutano muhimu ya kimataifa. Juhudi hizi za Rais wetu zimeipa Tanzania hadhi ya kuwa mwenyeji wa mikutano na vikao vya kimataifa ikiwemo Kongamano la Wanawake katika Biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara la Afrika mwezi Desemba 2023.
Mkutano wa Kimataifa wa Mifumo ya Chakula Afrika mwezi Septemba, 2023; Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mtaji wa Rasilimali Watu mwezi Julai, 2023; na Mkutano wa Mawaziri wa Afrika wanaosimamia masuala ya Fedha na Jinsia kuhusu uwekezaji kwa maendeleo ya wanawake na wasichana mwezi Novemba 2023. Hii ni baadhi tu.
ULINZI WA AMANI KIMATAIFA
Kufuatia uongozi thabiti na uwezeshaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, Tanzania imeendelea kutoa mchango katika ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Jukumu hili limeongeza sifa za nchi kimataifa, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali na kulipa jeshi letu uzoefu wa kimataifa. Hivi sasa wanajeshi wa Tanzania wanalinda amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia operesheni ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iitwayo SAMI DRC.
Katika nchi jirani ya Msumbiji nako Tanzania ikiwa sehemu ya SADC inalinda amani kupitia operesheni iitwayo SAMIM. Tanzania pia inashiriki katika operesheni ya kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kupitia operesheni ya MINUSCA na Lebanon kupitia operesheni ya UNIFIL.
USALAMA WA RAIA
Katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi likiwa na vitendea kazi, Mhe. Rais aliongeza bajeti yake kutoka Shilingi Bilioni 565 mwaka 2020/21 hadi Shilingi Bilioni 798 kwa mwaka 2023/24. Hivyo basi, magari 290 na pikipiki 105 zilinunuliwa na sasa zinatumika.
Aidha, jumla ya vituo 18 vya polisi na ofisi kumi za makamanda wa polisi wa mikoa nazo zimejengwa na majengo 20 ya madawati ya jinsia na watoto. Katika kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto, Polisi imeanzisha madawati 420 nchini kote.
Katika tatizo la uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi Jeshi la Polisi limefanikiwa kupokea silaha 1,785 na risasi 262 zilizosalimishwa na pia silaha 11,438 zimeteketezwa.