MKURUGENZI wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi, Advera Mwijage amesema, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wamefadhili ununuzi wa mashine tatu za kutengeneza makaa ya mawe zenye thamani Shilingi Bilioni 5.
Mhandishi Advera alisema hayo wakati wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia ambalo limekwenda sambamba na kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (2024) lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy.
Aidha, Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo alikuwa Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, Naibu Waziri wa Nishati.
“REA kwa kushirikiana na STAMICO imefadhili ununuzi wa mashine kubwa tatu kwa ajili ya kuzalisha makaa ya mawe. Mradi huo, umetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 5 na sisi kama Wakala tunahamasisha matumizi ya mkaa mbadala (Mkaa salama) kama chanzo cha nishati safi ya kupikia,” alisema Mhandisi, Advera.
Alisema, REA inatekeleza jukumu la kuhakikisha nishati za aina zote zinapatikana vijijini na kwa watu wote na kuongeza kuwa, imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia waendelezaji wa teknolojia za nishati safi pamoja na Miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia.
Mhandisi, Advera aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024, REA imetoa zaidi ya mitungi ya gesi ya kupikia 158,100 kwa Wananchi wa vijijini kama sehemu ya hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuongeza kuwa mitungi zaidi ya 400,000 itatolewa kupitia utaratibu huo.
Alisema, mbali na ugawaji wa mitungi ya gesi, REA imeanza kutekeleza programu ya kusambaza gesi asili kwa Wananchi wa vijijini wa mkoa wa Pwani na Lindi, Mradi huo una thamani ya Shilingi Bilioni 6.8 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi 980 zitaunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia kwenye nyumba zao.
Ameutaja Mradi mwingine ni wa kuwaunganisha Wananchi wa vijijini katika mkoa wa Pwani na Mtwara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Mradi huu una thamani ya Shilingi Bilioni 13.5 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi ya 1,400 zitanufaika.
Mhandisi, Advera alisema REA pia inatekeleza Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, ambapo Tanzania kuna magereza zaidi ya 129 ambapo imeelezwa kuwa matumizi ya kuni pekee yake ni zaidi ya asilimia 93. Mradi huo umeanza kutekelezwa na utagharimu Shilingi Bilioni 40.
Mradi mwingine unaofanana na huo ambao utaanza kutekelezwa hivi karibuni ni ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo kambi 26 zitanufaika, na zaidi ya Bilioni 3.5 zimetengwa.
Mradi wa mwisho ambao REA imepanga kuutekeleza ni wa kujenga miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye shule kongwe arobaini za sekondari hapa nchini, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Awali, Mgeni Rasmi Dkt. Philip Mpango, Dkt. Dotto Biteko, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga walitembelea banda la REA ambapo ujumbe mkubwa ulikuwa ni kuendelea kutoa hamasa na elimu ya matumizi ya tekonojia rahisi na nafuu kwa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia pamoja na kurahisisha katika upatikanaji wake.