MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda, yamelenga kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan katika sekta ya mafuta na gesi.
Mradi wa EACOP tayari umefungua fursa za ajira, biashara na uwekezaji kwa Watanzania. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati za Februari 2026, mradi umezalisha takribani ajira 10,000 katika kipindi cha ujenzi, huku zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zikipata zabuni za bidhaa na huduma zenye thamani ya zaidi ya Sh1.3 trilioni. Serikali pia imekusanya zaidi ya Sh70 bilioni kupitia ada, kodi na tozo mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa mradi.
Aidha, mradi huo umechangia uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika maeneo unayopita na unatarajiwa kuongeza shughuli za usafirishaji na biashara kupitia Tanga utakapoanza kufanya kazi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Meja Jenerali Marco Gaguti, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Mafuta na Gesi, Goodluck Shirima, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame.