Dkt. Nchimbi Katibu Mkuu mpya CCM

0

Na Jumbe Abdallah

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa imemteua Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo ambaye alijiuzulu.

Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.

Dkt. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)

Dkt. Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

Dkt. Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu, ambapo alipata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dkt. Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili.

Baada ya uchaguzi huo, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here