Walimu wakuu wasipokwe majukumu yao – Msonde

0
NAIBU Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde.

Na James Mwanamyoto, Sumbawanga

NAIBU Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amekemea kitendo cha baadhi ya viongozi wa halmashauri nchini kuwapoka wakuu wa shule jukumu la kusimamia miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule kwa kudhani kuwa hawana uwezo wa kusimamia miradi hiyo.

Dkt. Msonde amekemea tabia hiyo ya baadhi ya viongozi, wakati wa kikao kazi chake na viongozi wa mkoa na halmashauri kilicholenga kufanya tathmini na majumuisho ya ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani Rukwa.

Dkt. Msonde alisema uzoefu unaonesha kuwa, popote pale ambapo wakuu wa shule wamepokwa jukumu lao la kusimamia utekelezaji wa miradi, miradi hiyo haijakamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa na Serikali.

“Halmashauri haitekelezi wajibu wake wa kusimamia utendaji kazi wa mkuu wa shule na badala yake zinatekeleza yale ambayo yanapaswa kufanywa na kamati za manunuzi, kamati za mapokezi na usimamizi wa shule wakati ni kinyume na taratibu,” Dkt. Msonde alifafanua.

Dkt. Msonde ameanisha kuwa, Serikali ilipoamua kupeleka shuleni fedha za ujenzi wa miundombinu haikukosea kwani iliwapa hadhi wakuu wa shule kuwa maafisa masuuli, hivyo Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya wanaowajibu wa kuwalinda walimu wakuu wasipokwe majukumu yao ili kuilinda jukumu walilopewa.

Aliongeza kuwa, mwogozo wa kufanya manunuzi kwa kutumia Force Account umetoa mwelekeo kwa walimu wakuu wa namna ya kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na uundaji wa kamati mbalimbali zikiwemo za manunuzi na ujenzi ambazo miongoni mwa wajumbe wake ni wataalam wa manunuzi na wahandisi.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amefanya ziara ya kikazi mkoani Rukwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa aliyemtaka kwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here