Na Fauzia Mussa, MAELEZO
KATIBU Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Ali khamis Juma amesema watoto wenye ulemavu ni sehemu ya jamii na wanahitaji kupata fursa ya kuonesha vipaji vyao.
Akizungumza katika Bonanza la Michezo kwa watu wenye ulemavu huko viwanja vya Mao Zedon’g Katibu huyo alisema, watoto hao wanahaki ya kushiriki katika michezo kama watoto wengine hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika ili kuwasaidia kuipata haki hiyo.
Aidha, aliwataka Watendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili kuhakikisha watoto hao wanapata fursa za kushiriki katika mabonanza na kuonesha vipaji vyao.
Katibu Ali aliwapongeza wazazi walioongazana na watoto hao kwa kuwawezesha kushiriki michezo kwani bila ya mashirikiano yao wasingeweza kufika viwanjani hapo.
“Mtoto mwenye ulemavu hawezi kushiriki michezo kama wazazi wake hawapo tayari, nawashukuru wazazi waliowaleta watoto wao hapa na nashauri wazazi waliokaa majumbani kuwatoa watoto wao kwani wanahaki kama watoto wengine,” alisema Katibu huyo.
Hata hivyo aliwataka watu wenye ulemavu kushirikiana kwa pamoja ili kudai na kutetea haki zao kwa misingi ya amani.
“Nyinyi ni mashujaa msikubali kuonewa wala kudhulumiwa shikamaneni mdai kila haki yenu,” alisisitiza Katibu Ali.
Vile vile aliyataka Mabaraza ya Watu wenye Ulemavu ya Wilaya kuanzisha vilabu vya michezo katika Wilaya zao ili kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu kushiriki michezo kwani michezo hutoa fursa za ajira.
Akitoa maelezo mafupi Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Ussy Dede alisema bonaza hilo ni miongoni mwa shamrashamra kuelekea maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu ambayo huadimishwa kila ifikapo Disemba 3 Dunia kote.
Nao washiriki wa Bonanza hilo waliiomba jamii kuendelea kujifunza lugha za alama ili kuwasaidia watu wenye ulemavu wa uziwi kwani wamekuwa watu wa mwisho kupata taarifa.
Katika Bonanza hilo michezo mbalimbali ilichezwa na watu wenye ulemavu ikiwemo mbio fupi za Mita Mia, mbio za magunia, mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu wa viungo, kuvuta kamba, na nage.